Matendo 13

Matendo 13

Barnaba na Sauli wateuliwa

1Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kulelewa wa mfalme Herode, na Sauli.[#Mdo 11:27; #13:1 ‘Nigeri’ maana yake ‘mweusi’.]

2Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.[#Mdo 9:15]

3Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.[#Mdo 6:6; 14:23; 1 Tim 4:14; 5:22]

Mitume wahubiri katika Kipro

4Basi watu hao, walipotumwa hadi Kipro na Roho Mtakatifu wakateremkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro.[#Mdo 15:39]

5Na walipokuwa katika Salami wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi, nao walikuwa naye Yohana kuwa mtumishi wao.[#Mdo 12:12,25; 13:13]

6Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu;

7mtu huyu alikuwa pamoja na mtawala Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye mtawala akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu.

8Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule mtawala moyo wa kuiacha ile imani.[#2 Tim 3:8]

9Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho,

10akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyooka?[#Hos 14:9]

11Basi, angalia, mkono wa Bwana uko juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazungukazunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.[#Mdo 9:8; Yn 9:39]

12Ndipo yule mtawala, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.

Paulo na Barnaba wakiwa Antiokia ya Pisidia

13Kisha Paulo na wenziwe wakang'oa nanga wakasafiri kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohana akawaacha akarejea Yerusalemu.[#Mdo 12:12,25; 15:38]

14Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi.

15Kisha, baada ya Torati na kitabu cha Manabii kusomwa, wakuu wa sinagogi wakatuma mtu kwao, na kuwaambia, Ndugu, kama mkiwa na neno la kuwafaa watu hawa, lisemeni.[#Mdo 15:21]

16Paulo akasimama, akawapungia mkono, akasema, Enyi Waisraeli, nanyi mnaomcha Mungu, sikilizeni.[#13:16 Katika Kigiriki ni waume wa Israeli.]

17Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu, akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni katika nchi ya Misri, na kwa mkono ulioinuliwa akawatoa, akawaongoza.[#Kut 1:7; 12:51; Isa 1:2; Kut 6:1,6; 12:37,41; 14:8]

18Na kwa muda wa miaka kama arubaini akawavumilia katika jangwa.[#Hes 14:34; Kum 1:31; Kut 16:35]

19Na alipokwisha kuwaangamiza mataifa saba katika nchi ya Kanaani akawapa nchi yao iwe urithi kwa muda wa miaka kama mia nne na hamsini;[#Kum 7:1; Yos 14:1]

20baada ya hayo akawapa waamuzi hata wakati wa nabii Samweli.[#Amu 2:16; 1 Sam 3:20]

21Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila la Benyamini, kwa muda wa miaka arubaini.[#1 Sam 8:5; 10:21,24]

22Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.[#1 Sam 13:14; 16:12,13; Zab 89:20; Isa 44:28; Ebr 1:5; 5:5]

23Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi;[#2 Sam 7:12; Isa 11:1]

24Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiria watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake.[#Mk 1:4; Lk 3:3]

25Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mnadhani mimi ni nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake.[#Mt 3:11; Mk 1:7; Lk 3:16; Yn 1:20,27]

26Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Abrahamu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa.[#Zab 107:20; Mdo 13:46]

27Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu.[#Mdo 3:17; Yn 16:3]

28Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumwua wakamwomba Pilato auawe.[#Mt 27:22-23; Mk 15:13-14; Lk 23:21-23; Yn 19:15]

29Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamteremsha kutoka kwa ule mti, wakamweka kaburini.[#Mt 27:57-61; Mk 15:42-47; Lk 23:50-56; Yn 19:38-42]

30Lakini Mungu akamfufua katika wafu;[#Mdo 3:15]

31akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hadi Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu.[#Mdo 1:3]

32Na sisi tunawahubiria Habari Njema ya ahadi ile waliyopewa mababa,[#Mdo 13:23]

33ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili,[#Zab 2:7]

Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa.

34Tena ya kuwa alimfufua katika wafu, asipate kurudia uharibifu, amenena hivi,[#Isa 55:3]

Nitawapa ninyi mambo matakatifu ya Daudi yaliyo amini.

35Kwa hiyo anena na pengine,[#Zab 16:10; Mdo 2:27]

Hutamwachia Mtakatifu wako kuona uharibifu.

36Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu.[#1 Fal 2:10; Amu 2:10; Mdo 2:29]

37Bali huyu aliyefufuliwa na Mungu hakuona uharibifu.

38Basi, na ijulikane kwenu, ndugu zangu, ya kuwa kwa huyo mnahubiriwa msamaha wa dhambi;[#Mdo 10:43; Hes 15:30; Ebr 9:9; 13:20]

39na kwa yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa Torati ya Musa.[#Rum 10:4]

40Angalieni, basi, isiwajie habari ile iliyonenwa katika manabii.[#Hab 1:5]

41Tazameni, enyi mnaodharau,[#Hab 1:5]

kastaajabuni, mkatoweke;

kwa kuwa natenda kazi mimi siku zenu,

kazi ambayo msingeisadiki kabisa,

ijapo mtu akiwasimulia sana.

42Na walipokuwa wakitoka, wakawasihi waambiwe maneno haya sabato ya pili.

43Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakawafuata Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu.[#Mdo 11:23]

44Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu.

45Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana.[#Mdo 13:50; 14:2]

46Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona ninyi wenyewe kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa.[#Mdo 3:26; 18:6; Mt 10:6; Lk 7:30]

47Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana,[#Isa 42:6; 49:6]

Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa,

Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.

48Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.[#Mdo 11:18; Rum 8:29]

49Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote.

50Lakini Wayahudi wakawachochea wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao.

51Nao wakawakung'utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio.[#Mt 10:14; Mk 6:11; Lk 9:5; 10:11; Mdo 18:6]

52Lakini wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya