Matendo 14

Matendo 14

Paulo na Barnaba wakiwa Ikonio

1Ikawa huko Ikonio wakaingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi; na kwa vile walivyonena, kundi kubwa la Wayahudi na la Wagiriki wakaamini.

2Lakini Wayahudi wasioamini wakawataharakisha watu wa Mataifa na kuwatia nia mbaya juu ya ndugu.[#Mdo 13:45]

3Basi wakakaa huko wakati mwingi, wakinena kwa ushujaa katika Bwana, aliyelishuhudia neno la neema yake, akiwajalia ishara na maajabu yatendeke kwa mikono yao.[#Mdo 19:11; Mk 16:20; Ebr 2:4]

4Lakini jamii ya watu wa mjini wakafarakana; hawa walikuwa upande wa Wayahudi, na hawa upande wa mitume.

5Hata palipotokea shambulio la watu wa Mataifa na Wayahudi pamoja na wakubwa wao juu yao, kuwatenda jeuri na kuwapiga kwa mawe,[#Mdo 14:19; 2 Tim 3:11]

6wao wakapata habari wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia, na nchi zilizo kandokando;[#Mt 10:23]

7wakakaa huko, wakiihubiri Injili.[#Mdo 11:19,20]

Paulo na Barnaba wakiwa Listra na Derbe

8Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, asiyeweza kutumia miguu yake na aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa kwake.[#Mdo 3:2; 9:33; Yn 9:1]

9Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; naye Paulo akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa,[#Mdo 3:4; Mt 9:28]

10akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda.

11Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa lugha ya Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu.[#Mdo 28:6]

12Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji.

13Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng'ombe na mataji ya maua hadi malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na umati wa watu.

14Lakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika umati wa watu, wakipiga kelele,

15wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; tunawahubiria Habari Njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;[#Kut 20:11; Zab 146:6; Isa 37:16; Yer 32:17; Yak 5:17]

16ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe.[#Mdo 17:30]

17Lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha.[#Zab 147:8; Yer 5:24]

18Na kwa maneno hayo wakawazuia watu kwa shida, wasiwatolee dhabihu.

19Lakini Wayahudi wakafika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhania ya kuwa amekwisha kufa.[#2 Kor 11:25; 2 Tim 3:11]

20Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na kesho yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe.

Paulo na Barnaba warudi Antiokia ya Shamu

21Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia,[#Mt 28:19]

22wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwahimiza wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.[#Mdo 11:23; 1 The 3:3; Mt 7:14]

23Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini.[#Mdo 13:3]

24Wakapita kati ya Pisidia wakaingia Pamfilia.

25Na baada ya kuhubiri lile neno katika Perge wakateremka mpaka Atalia.

26Na kutoka huko wakaabiri kwenda Antiokia. Huko ndiko walikoombewa neema ya Mungu kwa ile kazi waliyokwisha kuitimiza.[#Mdo 13:1,2]

27Hata walipofika wakalikutanisha kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani.[#1 Kor 16:9; Mdo 11:18]

28Wakaketi huko wakati usiokuwa mchache, pamoja na wanafunzi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya