The chat will start when you send the first message.
1Ghasia ile ilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia.
2Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Ugiriki.
3Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia.
4Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberea, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia.[#Mdo 17:10; 19:29; Rum 16:21]
5Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa.[#Mdo 16:8]
6Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, baada ya safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba.
7Siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubia, maana aliazimia kusafiri siku iliyofuata, naye akafululiza maneno yake hadi usiku wa manane.[#1 Kor 16:2; Mdo 2:42,46]
8Palikuwa na taa nyingi katika ghorofa lile tulipokuwa tumekusanyika.
9Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka ghorofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa.
10Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake.[#1 Fal 17:21]
11Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hadi alfajiri, ndipo akaenda zake.
12Wakamleta yule kijana, akiwa mzima, wakafarijika faraja kubwa sana.
13Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimia kwenda kwa miguu.
14Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene.
15Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto.
16Kwa sababu Paulo alikusudia kusafiri pasipo kupitia Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana.[#Mdo 18:21]
17Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa.
18Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote,[#Mdo 18:19; 19:10]
19nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kutokana na njama za Wayahudi;[#Mdo 20:3]
20ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lolote liwezalo kuwafaa bali niliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba,
21nikiwashuhudia Wayahudi na Wagiriki wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.
22Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu nikiwa nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko;[#Mdo 19:21]
23isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja.[#Mdo 9:16; 21:4,11]
24Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.[#2 Tim 4:7; Mdo 21:13]
25Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huku na huko, hamtaniona uso tena.
26Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote.[#Mdo 18:6]
27Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.
28Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.[#Zab 74:2; 1 Tim 4:16; 1 Pet 5:2]
29Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi;[#Mt 7:15; 10:16; Yn 10:12]
30tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawafuatie wao.[#1 Yoh 2:19; Gal 4:17]
31Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi.[#Mk 13:35,37; 1 The 2:11]
32Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa.[#Kum 33:3]
33Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu.[#Mt 10:8; 1 Kor 9:12; 1 Sam 12:3]
34Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami.[#Mdo 18:3; 1 Kor 4:12; 1 The 2:9]
35Katika mambo yote nimewaonesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.
36Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote.[#Mdo 21:5]
37Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusubusu,[#Mdo 21:6; Rum 16:16; 1 Pet 5:14]
38wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.[#Mdo 20:25]