Matendo 7

Matendo 7

Hotuba ya Stefano kwa baraza

1Kuhani Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo?

2Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani,[#Mwa 12:1; Zab 29:3; Mwa 11:31; 15:7]

3akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonesha.[#Mwa 12:1; 48:4]

4Ndipo alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, akakaa Harani, akatoka huko baada ya kufa babaye, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa.[#Mwa 11:31; 12:4]

5Wala hakumpa urithi humu hata kiasi cha kuweka mguu; akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya uzao wake baadaye alipokuwa hana mtoto.[#Mwa 12:7; 13:15; 15:18; 17:8; 48:4; Kum 2:5]

6Mungu akanena hivi, ya kwamba wazawa wake watakuwa wageni katika nchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka mia nne.[#Mwa 15:13-14; Kut 2:22; 12:40]

7Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa.[#Kut 3:12]

8Akampa agano la tohara; basi Abrahamu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu.[#Mwa 17:10-14; 21:2-4; 25:26; 29:31—35:18]

9Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye,[#Mwa 37:11,28; 39:2,21; 45:4]

10akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote.[#Mwa 41:39-41; 39:21; Zab 105:21]

11Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha.[#Mwa 42:1-2; 41:54]

12Hata Yakobo aliposikia ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu mara ya kwanza.[#Mwa 42:2]

13Hata safari ya pili Yusufu akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusufu ikawa dhahiri kwa Farao.[#Mwa 45:1,3,16]

14Yusufu akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na watano.[#Mwa 45:9-10; 17:18; Mwa 46:27; Kut 1:5; Kum 10:22]

15Basi Yakobo akashuka mpaka Misri; akafa yeye na baba zetu;[#Mwa 46:1-7; 49:33; Kut 1:6]

16wakachukuliwa mpaka Shekemu wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Abrahamu alilinunua kwa kima fulani cha fedha kutoka kwa wana wa Hamori, huko Shekemu.[#Mwa 23:3-16; 33:19; 50:7-13; Yos 24:32]

17Basi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Abrahamu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri,[#Kut 1:7-8]

18hata mfalme mwingine asiyemfahamu Yusufu akaanza kutawala katika Misri.

19Huyo akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi.[#Kut 1:10-11,22; Mwa 24:7]

20Wakati huo akazaliwa Musa, naye alikuwa mzuri sana, akalelewa muda wa miezi mitatu katika nyumba ya babaye.[#Kut 2:2; Ebr 11:23]

21Wakati alipotupwa, binti Farao akamtwaa, akamlea awe kama mwanawe.[#Kut 2:3-10]

22Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo.

23Umri wake ulipokuwa kama miaka arubaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli.[#Kut 2:11-15]

24Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipizia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri.[#Kut 2:12]

25Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu.

26Kesho yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana?[#Kut 2:13]

27Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu?[#Kut 2:14; Lk 12:14]

28Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana?

29Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa kama mgeni katika nchi ya Midiani, akazaa wana wawili huko.[#Kut 2:15,22; 18:3-4]

30Hata miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima wa Sinai katika muali wa moto, kichakani.[#Kut 3:1-10; Kum 33:16]

31Musa alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia ili atazame, sauti ya Bwana ikamjia,

32Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akatetemeka, asithubutu kutazama.[#Kut 3:6]

33Bwana akamwambia, Vua viatu miguuni mwako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni nchi takatifu.[#Kut 3:5]

34Hakika nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nami nimeshuka niwatoe. Basi sasa, nitakutuma mpaka Misri.[#Kut 2:24; 3:7,10]

35Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka.[#Kut 2:14]

36Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika Bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arubaini.[#Kut 7:3,10; 14:21; Hes 14:33]

37Musa huyo ndiye aliyewaambia Waisraeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye.[#Kum 18:15,18; Mdo 3:22]

38Yeye ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea maneno ya uzima ili atupe sisi.[#Kut 19:1—20:17; Kum 5:1-33; Mdo 7:53; Kum 9:10]

39Mtu huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, na kwa mioyo yao wakarejea Misri,[#Hes 14:3]

40wakamwambia Haruni, Tutengenezee miungu, watakaotutangulia; maana huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui lililompata.[#Kut 32:1,23]

41Wakatengeneza ndama siku zile, wakaleta dhabihu kwa sanamu ile, wakafurahia kazi za mikono yao.[#Kut 32:2-6]

42Basi Mungu akaghairi, akawaacha ili waliabudu jeshi la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii,[#Amo 5:25-27; Yer 19:13]

Je! Mlinitolea mimi dhabihu na sadaka

Miaka arubaini katika jangwa, enyi nyumba ya Israeli?

43Nanyi mlichukua hema ya Moleki,

Na nyota za mungu wenu Refani,

Sanamu mlizozifanya ili kuziabudu;

Nami nitawafahamisha mwende mbali kupita Babeli.

44Ile hema ya ushahidi ilikuwa pamoja na baba zetu jangwani, kama alivyoagiza yeye aliyesema na Musa, ya kwamba aifanye kulingana na mfano ule aliouona;[#Kut 25:9,40]

45ambayo baba zetu, kwa kupokezana, wakaiingiza pamoja na Yoshua katika milki ya Mataifa wale, ambao Mungu aliwafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Daudi;[#Yos 3:14-17; 18:1; Mwa 17:8; 48:4; Kum 32:49]

46aliyepata fadhili mbele za Mungu, naye aliomba ampatie Mungu wa Yakobo maskani.[#2 Sam 7:1-16; 1 Nya 17:1-14; Zab 132:5]

47Lakini Sulemani alimjengea nyumba.[#1 Fal 6:1-38; 2 Nya 3:1-17]

48Ila Yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizojengwa kwa mikono, kama vile asemavyo nabii,[#Isa 66:1,2]

49Mbingu ni kiti changu cha enzi,[#Isa 66:1-2]

Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu;

Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana,

50Au ni mahali gani nitakapostarehe?

Si mkono wangu uliofanya haya yote?

51Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.[#Isa 63:10; Kut 32:9; Law 26:41; Hes 27:14; Yer 9:26]

52Ni yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, mkamwua;[#2 Nya 36:16; Mt 23:31]

53ninyi mlioipokea torati kwa agizo la malaika msiishike.[#Kut 20:1-26; Gal 3:19; Ebr 2:2]

Kupigwa mawe kwa Stefano

54Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno.[#Mdo 5:33]

55Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kulia wa Mungu.[#Lk 22:69]

56Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kulia wa Mungu.

57Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,

58wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.[#Mdo 22:20]

59Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu.[#Zab 31:5; Lk 23:46]

60Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona kitendo cha kuuawa kwake kuwa sawa.[#Lk 23:34]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya