Amosi 8

Amosi 8

Kikapu cha Matunda

1Haya ndiyo aliyonionesha Bwana MUNGU; tazama, kikapu cha matunda ya wakati wa joto.

2Akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona kikapu cha matunda ya wakati wa joto. Ndipo BWANA akaniambia, Mwisho wao watu wangu Israeli umewajia; sitawapita tena kamwe.[#Yer 1:12; Omb 4:18; Eze 7:2]

3Tena nyimbo za hekaluni zitakuwa vilio siku ile, asema Bwana MUNGU; mizoga itakuwa mingi; kila mahali wataitupa, wakinyamaza kimya.

4Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi,

5mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini, tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandaa ngano? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu;[#Neh 13:15; Mik 6:10]

6tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano.

7BWANA ameapa kwa fahari ya Yakobo, Hakika sitazisahau kamwe kazi zao hata mojawapo.[#Zab 68:34; Hos 8:13]

8Kwa ajili ya hayo, je! Haitatetemeka nchi, na kuomboleza kila mtu akaaye ndani yake? Naam, itainuka yote pia kama huo Mto; nayo itataabika na kupwa tena kama Mto wa Misri.[#Hos 4:3; Amo 9:5]

9Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana MUNGU, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, nami nitaitia nchi giza wakati wa nuru ya mchana.[#Ayu 5:14; Isa 13:10; Yer 15:9; Amo 4:13; Mik 3:6; 1 The 5:2,3]

10Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upara katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu.[#Yer 6:26; Zek 12:10; Lk 7:12,13]

11Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya BWANA.[#1 Sam 3:1; Zab 74:9; Eze 7:26; Mik 3:6]

12Nao watatangatanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huku na huko, kulitafuta neno la BWANA, wasilione.

13Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu.

14Na hao waapao kwa dhambi ya Samaria, na kusema, Kama aishivyo Mungu wako, Ee Dani, na, Kama iishivyo njia ya Beer-sheba, hao nao wataanguka, wasiinuke tena.[#Kum 9:21; 1 Fal 12:30; Hos 8:5,6; 10:5; Mik 1:5]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya