Baruku 1

Baruku 1

DIBAJI

Baruku na Wayahudi katika Babeli

1Haya ni maneno ambayo Baruku mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, mwana wa Sedekia, mwana wa Asadia, mwana wa Hilkia,[#Yer 36:4]

2aliyaandika huko Babeli katika mwaka wa tano, siku ya saba ya mwezi; ndio wakati Wakaldayo walioteka Yerusalemu wakauteketeza kwa moto.

3Naye Baruku aliyasoma maneno ya kitabu hiki katika masikio ya Yekonia mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, na katika masikio ya watu wote waliokuja kwenye masomo,[#2 Fal 24:8-17]

4na katika masikio ya wakuu na ya wana wa mfalme na wazee, na katika masikio ya watu wote wadogo kwa wakubwa, yaani wote waliokuwa wakikaa Babeli kando ya mto Sudi.

5Nao wakalia na kufunga na kuomba mbele ya BWANA;

6tena walifanya mchango wa fedha kwa kadiri ya uwezo wa kila mtu,

7wakaipeleka Yerusalemu kwa kuhani mkuu, Yoakimu mwana wa Hilkia, mwana wa Shalumu, na kwa makuhani, na wote waliokuwapo pamoja naye Yerusalemu wakati ule.

8Ndio wakati alipovichukua vyombo vya nyumba ya BWANA vilivyotwaliwa kutoka hekaluni, na kuvirudisha katika nchi ya Yuda, siku ya kumi ya mwezi Siwani. Navyo ni vile vyombo vya fedha ambavyo Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda,

9alivyovifanyiza baada ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, kumchukua Yekonia na wakuu wa nchi, na mateka, na mashujaa, na wenyeji wa nchi, kutoka Yerusalemu na kuwaleta Babeli.

Barua kwa Yerusalemu

10Wakasema, Tazameni, tumewaletea fedha, nanyi kwa fedha hiyo nunueni sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za dhambi, na uvumba, mtengeneze dhabihu mkaitoe katika madhabahu ya BWANA Mungu wetu,

11na kumwombea Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na Belshaza mwanawe, wapate uzima, siku zao ziwe nyingi kama zilivyo siku za mbingu juu ya nchi.

12Naye BWANA atatupa nguvu, na kututia nuru macho yetu, nasi tutakaa chini ya uvuli wa Nebukadreza mfalme wa Babeli, na chini ya uvuli wa Belshaza mwanawe, na kuwatumikia siku nyingi, na kupata kibali machoni pao.

13Na mtuombee kwa Bwana MUNGU wetu, maana tumemtenda dhambi Bwana MUNGU wetu, na hata leo ghadhabu ya BWANA na hasira yake haijatugeukia mbali.

14Nanyi mtakisoma kitabu hiki ambacho tumewaletea, kuungama katika nyumba ya BWANA wakati wa sikukuu na siku za kusanyiko takatifu.

15Nanyi mtasema hivi.

SALA YA WAHAMISHWA

Kuungama dhambi

Kwa Bwana MUNGU wetu, haki; lakini kwetu sisi haya ya uso kama hivi leo, kwa watu wa Yuda na kwa wenyeji wa Yerusalemu,

16na kwa wafalme wetu, na kwa wakuu wetu, na kwa makuhani wetu, na kwa manabii wetu, na kwa baba zetu,

17kwa sababu tumetenda dhambi mbele ya BWANA.

18Tumemwasi, wala hatukuitii sauti ya Bwana MUNGU wetu, kwenda katika sheria zake alizoziweka mbele yetu.

19Tangu siku BWANA aliyowatoa baba zetu katika nchi ya Misri hata leo tumemwasi Bwana MUNGU wetu na kutenda yasiyofaa kwa kutokuisikiliza sauti yake.

20Kwa hiyo mapigo haya yameshikamana nasi, na ile laana ambayo BWANA alimwamuru mtumishi wake Musa, katika siku aliyowaleta baba zetu kutoka katika nchi ya Misri ili atupe nchi ijaayo maziwa na asali, kama hivi leo.[#Kum 28:15-68]

21Lakini hatukuisikiliza sauti ya Bwana MUNGU wetu, kwa kuyafuata maneno yote ya manabii aliyotupelekea,

22bali tulikwenda kila mtu katika mawazo ya moyo wake mbaya, kutumikia miungu ya kigeni na kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana MUNGU wetu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya