Baruku 3

Baruku 3

1Ee Bwana Mwenyezi, MUNGU wa Israeli; moyo uliotaabika, roho iliyolegea, inakulilia.

2Sikia, Ee BWANA, na kuturehemu, kwa kuwa ndiwe BWANA mwenye rehema; naam, uturehemu sisi, kwa kuwa tumetenda dhambi mbele yako.

3Wewe umeketi hali ya mfalme milele, na sisi tunapotea kila siku.

4Ee Bwana Mwenyezi, MUNGU wa Israeli, yasikilize sasa maombi ya Waisraeli na ya wana wa wale waliotenda dhambi mbele yako, wasioisikiliza sauti yako Wewe Mungu wao, na kwa sababu hiyo mapigo haya yametushika.

5Usiyakumbuke maovu ya baba zetu, bali ukumbuke sasa uweza wako na jina lako.

6Maana Wewe ndiwe Bwana MUNGU wetu, nasi tutakuhimidi Wewe, Ee BWANA.

7Ndiyo sababu umetutia kicho chako mioyoni, ili tupate kuliitia jina lako. Nasi tutakuhimidi katika uhamisho wetu, kwa kuwa tunaukumbuka uovu wote wa baba zetu waliokutenda dhambi.

8Tazama, tumo utumwani hata leo huku ulikotutawanya, kuwa lawama na laana, na chini ya hukumu, kwa ajili ya uovu wa baba zetu waliomwasi Bwana MUNGU wetu.

HEKIMA, THAWABU YA PEKEE YA ISRAELI

Kusifu hekima

9Sikia, Ee Israeli, amri za uzima,[#Mit 4:20-22]

Tega sikio lako kujua hekima.

10Imekuwaje, Ee Israeli,

Uko katika nchi ya adui zako,

Ukizeeka katika nchi ya kigeni?

11Umetiwa najisi na wafu,

Umehesabiwa nao washukao shimoni?

12Umeiacha chemchemi ya uzima.

13Maana kama ungaliifuata njia ya Mungu

Ungalikaa kwa amani siku zote.

14Itafute hekima ilipo, na nguvu, na maarifa,

Ili ujue ulipo wingi wa siku, na uzima.

Ilipo nuru ya macho na amani.

15Ni nani aliyeona mahali pake?[#Ayu 28:12,20]

Na kuingia katika ghala zake?

16Wako wapi wakuu wa mataifa,

Nao waliotumikisha wanyama wa nchi

17Na kucheza na ndege za angani?

Wao walioweka akiba ya fedha na dhahabu

Ambayo wanadamu huitumainia

Wala hawaishi kuitafuta?

18Wao waliotafuta fedha kwa uangalifu mwingi,

Ambao kazi zao hazitafutikani,

19Wametoweka na kushuka kaburini,

Na wengine wameinuka mahali pao.

20Wadogo wao waneona nuru

Na kukaa katika nchi.

Lakini njia ya hekima hawakuijua

21Wala kuyafahamu mapito yake.

Watoto wao nao hawakuishika,

Wako mbali na njia yake.

22Haikujulikana huko Kanaani,

Wala kuonekana katika Temani.

23Wana wa Agari, watafutao maarifa duniani,

Wachuuzi wa Midiani na Tema,

Watungaji wa hadithi na wachunguzi wa elimu

Katika hao wote hakuna aliyeitambua njia ya hekima,

Wala kuyakumbuka mapito yake.

24Ee Israeli, jinsi ilivyo kuu nyumba ya Mungu,

Na jinsi inavyoenea milki yake!

25Ni kubwa, haina mpaka;

juu, haipimiki.

26Huko walizaliwa mashujaa waliosifiwa zamani,[#Mwa 6:4; Hek 14:6]

Warefu mno, hodari wa vita.

27Mungu hakuwachagua hao,

Wala kuwapa hao njia ya maarifa.

28Kwa hiyo walipotea kwa kukosa hekima,

Walipotea kwa ujinga wao wenyewe.

29Ni nani aliyepanda mbinguni na kuishika,

Na kuishusha kutoka mawinguni?

30Ni nani aliyevuka bahari kuitafuta

Na kuipata kwa dhahabu safi?

31Hakuna aijuaye njia yake

Wala kuyafahamu mapito yake.

32Lakini Yeye ajuaye yote anaijua,

Aliitambua kwa ufahamu wake.

Yeye aliyeweka dunia milele

Na kuijaza wanyama wenye miguu minne.

33Yeye aitumaye nuru ikaenda,

Akaiita ikamtii kwa kicho.

34Nyota zikang'aa katika majira yake zikafurahi.

35Alipoziita zilisema, Tupo hapa!

Na kwa furaha zikamng'aria Muumba wao.

36Huyu ndiye Mungu wetu, wala hakuna afananaye naye.

37Ameivumbua njia yote ya hekima

Akampa Yakobo mtumishi wake na Israeli mpendwa wake.

38Baadaye hekima ikaonekana duniani

Ikakaa na watu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya