The chat will start when you send the first message.
1Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi katika mkono wa kulia wa Mungu.[#Zab 110:1; Kol 2:12]
2Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.[#Mt 6:33]
3Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.[#Rum 6:2]
4Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.[#1 Kor 15:43; Flp 1:21; Gal 2:20]
5Basi, viueni viungo vyenu vilivyo vya kidunia, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;[#Rum 6:6; 8:13; Efe 4:19; 5:3,5]
6kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu.[#Efe 5:6]
7Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo.
8Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na masuto, na matusi vinywani mwenu.[#Efe 4:25-31; 5:4]
9Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake;[#Efe 4:22]
10mkivaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu kulingana na mfano wake yeye aliyeuumba.[#Mwa 1:26; Efe 4:24]
11Hapo hapana Mgiriki wala Myahudi, kutahiriwa wala kutotahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala muungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote.[#Gal 3:28]
12Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu,[#Efe 4:2,32; 5:2; 1 Pet 2:9]
13mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.[#Efe 4:32; 5:2; Mt 6:14]
14Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.[#Rum 13:8,10; Efe 4:3]
15Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.[#Efe 4:4; Flp 4:7; 1 Kor 12:13,27]
16Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.[#Efe 5:19-20]
17Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kupitia kwake.[#1 Kor 10:31; Efe 5:20]
18Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana.[#Efe 5:22—6:9; 1 Pet 3:1]
19Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao.[#Efe 5:25; 1 Pet 3:7]
20Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana.[#Efe 6:1]
21Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.[#Efe 6:4]
22Ninyi watumwa, watiini hao ambao kwa mwili ni bwana zenu, katika mambo yote, si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana.[#Efe 6:5-8]
23Lolote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu,
24mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo.
25Maana adhulumuye atapata mapato ya udhalimu wake, wala hakuna upendeleo.[#Kum 10:17; Rum 2:11; Efe 6:9]