The chat will start when you send the first message.
1Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati huo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile.[#Ufu 16:18; Isa 11:11; Yer 30:7; Hos 3:5; Yoe 3:16; Rum 11:26; Kut 32:32; Isa 4:3; Eze 13:9; Lk 10:20; Mt 24:21; Mk 13:19; Ufu 7:14; 12:7]
2Tena, wengi wa hao wanaolala katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.[#Isa 26:19; Mt 25:46; Yn 5:29]
3Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.[#1 Kor 15:41]
4Lakini wewe, Ee Danieli, yafunge maneno haya, ukakitie mhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huku na huko, na maarifa yataongezeka.[#Ufu 22:10]
5Ndipo mimi, Danieli, nikatazama, na kumbe, wamesimama wengine wawili, mmoja ukingoni mwa mto upande huu, na mmoja ukingoni mwa mto upande wa pili.
6Na mmoja akamwuliza yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, Je! Itakuwa muda wa miaka mingapi hata mwisho wa mambo haya ya ajabu?[#Zab 74:9; 1 Pet 1:12; Ufu 6:10]
7Nami nikamsikia yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, hapo alipoinua mkono wake wa kulia na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni; akaapa kwa yeye aliye hai milele na milele, ya kwamba itakuwa nyakati tatu na nusu; tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu, ndipo mambo hayo yote yatakapotimizwa.[#Dan 7:25; Lk 21:24; Ufu 10:5; 12:14]
8Nami nikasikia, lakini sikuelewa; ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, mwisho wa mambo haya utakuwaje?
9Akasema, Nenda zako, Danieli; maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa mhuri, hata wakati wa mwisho.
10Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa.[#Zek 13:9; Yn 7:17; Ufu 22:11]
11Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini.[#Dan 9:27; 11:31; Mt 24:15; Mk 13:14]
12Heri angojaye, na kuzifikia siku hizo elfu na mia tatu na thelathini na tano.
13Lakini nenda zako hata utakapokuwa mwisho ule; maana wewe utastarehe, nawe utaamka katika kura yako mwisho wa siku hizo.[#Isa 57:2; Zab 1:5]