The chat will start when you send the first message.
1Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,[#2 The 2:9]
2ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;[#Yer 28:9; Mt 7:22]
3wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda BWANA, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.[#Mt 24:24; 1 Kor 11:19; 2 The 2:11; Ufu 13:14]
4Tembeeni kwa kumfuata BWANA, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.[#2 Fal 23:3; 2 Nya 34:31; 1 Yoh 1:7; 2 Yoh 1:6]
5Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya BWANA, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru BWANA, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako.[#1 Fal 18:40; Isa 9:15,16; Yer 14:15; Zek 13:3; Ufu 19:20; 2 Fal 10:18-28; 1 Kor 5:13]
6Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mama yako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako;[#Ayu 2:9; Mik 7:5]
7katika miungu ya mataifa yaliyo kandokando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia;
8usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche;[#Kut 20:3; Mit 1:10; Gal 1:8,9; 1 Yoh 5:21]
9mwue kweli; mkono wako na uwe wa kwanza juu yake katika kumwua, na baadaye mikono ya watu wote.[#Kum 17:7; Mdo 7:58]
10Nawe mtupie mawe hata afe; kwa kuwa alitaka kukupotoa na BWANA, Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.
11Na Israeli wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako.[#Kum 19:20]
12Ukisikia yasemwa habari ya miji yako mmojawapo, akupayo BWANA, Mungu wako, ukae humo, ukiambiwa,[#Yos 22:11; Amu 20:1]
13Kumetoka katikati yako mabaradhuli kadha wa kadha, wamewapotoa wenyeji wa mji wao, wakisema, Twendeni tukaabudu miungu mingine msiyoijua;[#1 Sam 2:12; 2 Kor 6:15; 1 Yoh 2:19; Yud 1:19; 2 Fal 17:21]
14ndipo nawe uulize na kutafuta, ukiuliza kwa bidii; nawe angalia, ikiwa kweli, na jambo lile halina shaka, kwamba machukizo mfano wa haya yafanyika katikati yako;
15hakika yako uwapige wenyeji wa mji ule kwa makali ya upanga, kwa kuwaangamiza kabisa, pamoja na vitu vyote vilivyomo, na wanyama walio humo, kwa makali ya upanga.[#Yos 6:17]
16Na nyara zake zote uzikusanyie katikati ya njia yake; na mji uuteketeze kwa moto, na nyara zake zote, kuwe sadaka kamili ya kuteketezwa kwa BWANA, Mungu wako; nao utakuwa magofu milele; usijengwe tena.[#Yos 8:28; Isa 17:1; 25:2; Yer 49:2]
17Kisishikamane na mkono wako kitu chochote katika kitu kilichoharimishwa; ili ageuke BWANA na ukali wa hasira zake akurehemu, akuonee huruma, na kukufanya kuwa wengi, kama alivyowaapia baba zako;[#Kum 7:26; Yos 6:18; 7:1,11,12; 6:26; Mwa 22:17; 26:4,24]
18utakaposikiza sauti ya BWANA, Mungu wako kwa kushika maagizo yake yote nikuagizayo leo, ufanye yaliyoelekea machoni pa BWANA, Mungu wako.[#Kum 12:25; Mt 6:33; 7:21,24]