Kumbukumbu la Torati 27

Kumbukumbu la Torati 27

Mawe yenye maandishi na madhabahu katika mlima

1Musa na wazee wa Israeli wakawaagiza wale watu wakawaambia, Shikeni maagizo yote niwaagizayo leo.

2Na iwe, siku mtakayovuka Yordani kwenda nchi akupayo BWANA, Mungu wako, ujisimamishie mawe makubwa, ukayatalize matalizo,[#Yos 4:1; 8:30-32]

3uyaandike maneno yote ya torati hii juu yake, utakapokwisha kuvuka; ili upate kuingia nchi akupayo BWANA, Mungu wako, nchi imiminikayo maziwa na asali, kama alivyokuahidi BWANA, Mungu wa baba zako.

4Na iwe, mtakapokwisha vuka Yordani myasimamishe mawe haya, niwaagizayo hivi leo, katika mlima Ebali, nawe yatalize matalizo.[#Kum 11:29; Yos 8:30]

5Na huko umjengee madhabahu BWANA, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu yake.[#Kut 20:25; Yos 8:31]

6Jenga hiyo madhabahu ya BWANA, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa; ukamtolee BWANA, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake;

7ufanye na sadaka za amani, ukale huko; nawe furahi mbele za BWANA, Mungu wako.

8Kisha, andika juu ya mawe hayo maneno ya torati hii yote, waziwazi sana.[#Hab 2:2]

9Musa na makuhani Walawi wakawaambia Israeli wote wakasema, Nyamaza, usikize, Ee Israeli; leo umekuwa watu wa BWANA, Mungu wako.

10Basi isikize sauti ya BWANA, Mungu wako, ufanye maagizo yake na amri zake nikuagizavyo leo.

11Musa akawaagiza wale watu siku iyo hiyo, akasema,

12Hawa na wasimame juu ya mlima wa Gerizimu kwa kuwabarikia watu, mkiisha vuka Yordani; Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Yusufu, na Benyamini;[#Kum 11:29; Yos 8:33-35; Amu 9:7]

13na hawa na wasimame juu ya mlima wa Ebali kwa laana; Reubeni, na Gadi, na Asheri, na Zabuloni, na Dani, na Naftali.

14Kisha Walawi na wajibu, wawaambie watu wote wa Israeli kwa sauti kuu,[#Kum 33:10; Yos 8:33; Neh 8:7,8; Dan 9:11; Mal 2:7-9]

15Na alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga, au ya kusubu, machukizo kwa BWANA, kazi ya mikono ya fundi, akaisimamisha kwa siri. Na watu wote wajibu, waseme, Amina.[#Kut 20:4; 34:17; Law 19:4; 26:1; Kum 4:15-18; 5:8; Isa 44:9; Hos 13:2; Hes 5:22; Yer 11:5; 1 Kor 14:16]

16Na alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake. Na watu wote waseme, Amina.[#Kut 20:12; Kum 5:16; Law 19:3]

17Na alaaniwe aondoaye mpaka wa jirani yake. Na watu wote waseme, Amina.[#Kum 19:14; Mit 22:28]

18Na alaaniwe ampotezaye kipofu akakosa njia. Na watu wote waseme, Amina.[#Law 19:14; Ayu 29:15; Mit 28:10; Mt 15:14; Ufu 2:14]

19Na alaaniwe apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe. Na watu wote waseme, Amina.[#Kut 22:21; 23:9; Law 19:33-34; Kum 10:18; 24:17-18; Mal 3:5]

20Na alaaniwe alalaye na mke wa baba yake, kwa kuwa amefunua mavazi ya babaye. Na watu wote waseme, Amina.[#Law 18:8; 20:11; Kum 22:30; 1 Kor 5:1]

21Na alaaniwe alalaye na mnyama wa aina yoyote. Na watu wote waseme, Amina.[#Kut 22:19; Law 18:23; 20:15]

22Na alaaniwe alalaye na dada yake, binti ya babaye, au binti ya mamaye. Na watu wote waseme, Amina.[#Law 18:9; 20:17; 2 Sam 13:1]

23Na alaaniwe alalaye na mkwewe, mamaye mkewe. Na watu wote waseme, Amina.[#Law 18:17; 20:14]

24Na alaaniwe ampigaye mwenzake kwa siri. Na watu wote waseme Amina.[#Law 24:17; Hes 35:31]

25Na alaaniwe atwaaye ujira wa kumwua asiye makosa. Na watu wote waseme, Amina.[#Kut 23:7; Kum 10:17; 16:19; Zab 15:5; Eze 22:12]

26Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, Amina.[#Gal 3:10; Zab 119:21; Yer 11:3]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya