Kumbukumbu la Torati 28

Kumbukumbu la Torati 28

Baraka za utiifu

1Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;[#Kum 11:13-17; Kut 15:26; Law 26:3; Zab 106:3; 111:10; Isa 1:19; 3:10; Yer 11:4; 12:16; 1 Nya 14:2; Rum 2:10]

2na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako.[#Zek 1:6]

3Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.[#Zab 128:1,4; Mwa 39:5]

4Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, kuongezeka kwa ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo wako.[#Mwa 22:17; 1 Tim 4:8]

5Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.

6Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo.[#Zab 121:8]

7BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.[#2 Sam 22:38]

8BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako.[#Law 25:21; Mit 3:10; Kum 15:10]

9BWANA atakuweka uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia; utakaposhika maagizo ya BWANA, Mungu wako, na kutembea katika njia zake.[#Mwa 17:7; Kut 19:5; Isa 1:26; 62:12; Tit 2:14]

10Na mataifa yote ya duniani watakuona umeitwa kwa jina la BWANA, nao watakuwa na hofu kwako.[#2 Nya 7:14]

11BWANA atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi BWANA aliyowaapia baba zako kwamba atakupa.[#Mit 10:22]

12Atakufunulia BWANA hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.[#Yak 1:18]

13BWANA atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya;

14msipokengeuka katika maneno niwaamuruyo leo kwa lolote, kwenda mkono wa kulia wala wa kushoto, kwa kuifuata miungu mingine na kuitumikia.[#Yos 1:7; 2 Fal 22:2; Mit 4:27]

Maonyo juu ya Kutotii

15Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.[#Law 26:14; Omb 2:17; Dan 9:11; Mal 2:2; Rum 2:8,9]

16Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.

17Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.

18Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, kuongezeka kwa ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo wako.[#Isa 3:1; Hab 3:17]

19Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,

20BWANA atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.[#Mit 3:33; Zek 5:3,4; Mal 2:2; Zab 80:16; Isa 30:17; 51:20]

21BWANA atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki.[#Law 26:25; Hes 14:12; Yer 16:4; 24:10; Amo 4:10; Mt 24:7]

22BWANA atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa joto jingi, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie.[#Law 26:16]

23Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma.

24BWANA atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie.

25BWANA atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huku na huko katika falme zote za duniani.[#Law 26:17; Kum 32:30; Isa 30:17; Yer 15:4; 24:9; Eze 23:46]

26Na mzoga wako utakuwa chakula cha ndege wote wa angani, na wanyama wote wa duniani, pasiwe na mtu wa kuwafukuza.

27BWANA atakupiga kwa majipu ya Misri, na kwa bawasiri, na kwa pele, na kwa kujikuna, ambayo hupati kupoa.[#Kut 9:9; 15:26; 1 Sam 5:6; Zab 78:66]

28BWANA atakupiga kwa wazimu, na kwa upofu, na kwa bumbuazi la moyoni;

29utakwenda kwa kupapasapapasa mchana, kama apapasavyo kipofu gizani, wala hufanikiwi katika njia zako; nawe sikuzote utaonewa na kutekwa nyara, wala hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.

30Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.[#Ayu 31:10; Yer 8:10]

31Ng'ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang'anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo wako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa.

32Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako.

33Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima;[#Law 26:16; Yer 5:17]

34hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona.

35BWANA atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa.

36BWANA atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe.[#2 Fal 17:4; 24:12,14; Yer 39:1; 2 Nya 33:1; 36:1; Yer 16:13]

37Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza BWANA.[#1 Fal 9:7,8; Yer 24:9; 25:9; Zek 8:13; Zab 44:14]

38Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila.[#Mik 6:15; Hag 1:6; Kut 10:4; Yoe 1:4]

39Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu.

40Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika.

41Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani.[#Yer 52:28]

42Miti yako yote, na mazao ya nchi yako, nzige watakuwa nayo.

43Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini.

44Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.[#Ezr 9:7; Omb 1:5]

45Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza;

46nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele;[#Hes 26:10; Isa 8:18; Eze 5:15; 14:8]

47kwa kuwa hukumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote;[#Neh 9:35-37]

48kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta BWANA juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza.[#Isa 47:6; Yer 27:12; 28:14; Mt 11:29]

49BWANA atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usiloufahamu ulimi wake;[#Yer 5:15; 6:22,23; Lk 19:43; Yer 48:40; 49:22; Omb 4:19; Eze 17:3; Hos 8:1]

50taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana;[#Dan 8:23; 2 Nya 36:17; Isa 47:6]

51naye atakula uzao wa ng'ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala kuongezeka kwa ng'ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza.[#Isa 1:7; 62:8; Yer 5:15-17]

52Naye atakuhusuru katika malango yako yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila upande, katika nchi yako yote aliyokupa BWANA, Mungu wako.[#2 Fal 25:1; Yer 37:8; Mt 22:7]

53Nawe utakula uzao wa tumbo lako mwenyewe, nyama ya wana wako na binti zako aliokupa BWANA, Mungu wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako.[#Law 26:29; 2 Fal 6:28,29; Yer 19:9; Omb 2:20; 4:10; Lk 21:23]

54Mtu mume kati yenu aliye mwororo na laini sana, jicho lake litakuwa ovu juu ya nduguye, na juu ya mke wa kifuani mwake, na juu ya masalio ya wanawe waliosalia naye;

55hata asitake wao mmojawapo apewe katika nyama ya wanawe atakaowala, kwa kuwa hana kitu kilichomsalia kwake; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako yote.

56Mwanamke kati yenu aliye mwororo na laini, ambaye hangehatarisha kuweka wayo wa mguu wake nchi kwa umalidadi na ulaini, jicho lake huyu litakuwa ovu juu ya mume wa kifuani mwake, na juu ya mwanawe, na juu ya binti yake,

57na juu ya mchanga wake atokaye katikati ya miguu yake, na juu ya wanawe atakaowazaa; kwa kuwa atawala kwa siri, kwa uhitaji wa vitu vyote; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako.[#2 Fal 6:28-29; Omb 4:10]

58Kama hutaki kutunza kufanya maneno yote ya torati hii yaliyoandikwa katika kitabu hiki, upate kulicha jina hili la fahari na utisho, BWANA, MUNGU WAKO;[#Kut 6:3; Zab 99:3; Isa 57:15; 29:23; Mal 1:14; Zab 20:1; 83:18; Isa 42:8; Mal 2:3; 4:2; Flp 2:10]

59ndipo atakapofanya BWANA mapigo yako yawe ya ajabu, na mapigo ya uzao wako, mapigo makubwa kwa kweli, ya kudumu sana, na magonjwa mazito ya kudumu sana.[#1 Fal 9:7,9; Omb 1:9,12; 4:12; Dan 9:12; 2 Nya 21:12-15]

60Naye atakurejezea maradhi yote ya Misri juu yako uliyokuwa ukiyaogopa, nayo yataambatana nawe.

61Tena kila ugonjwa, na kila pigo yasiyoandikwa katika kitabu cha Torati hii, atakutia nayo BWANA juu yako, hata utakapokwisha kuangamizwa.

62Nanyi mtasalia wachache kwa hesabu, ninyi mliokuwa mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi; kwa kuwa hukuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako.[#Neh 9:23]

63Tena itakuwa, kama vile alivyokuwa akifurahi BWANA juu yenu kwa kuwatendea mema na kuwafanya kuwa wengi, ndivyo atakavyofurahi BWANA juu yenu kwa kuwapoteza na kuwaangamiza; nanyi mtanyakuliwa katika hiyo nchi mwingiayo kuimiliki.[#Isa 62:5; Yer 32:41; Mik 7:18; Sef 3:17; Lk 15:6,10; Mit 1:26; Isa 1:24]

64BWANA atakutawanya katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata ncha hii ya dunia; nawe huko utatumikia miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako, nayo ni miti na mawe.[#Law 26:33; Neh 1:8; Yer 16:13]

65Wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote, wala hutakuwa na kituo cha wayo wa mguu wako; lakini BWANA atakupa huko moyo wa kutetema, na macho ya kuzimia, na roho ya kudhoofika;[#Mwa 8:9; Isa 57:21; Eze 5:12,17; Amo 9:4; Law 26:36]

66na uzima wako utakuwa na wasiwasi mbele yako; nawe utakuwa na woga usiku na mchana, wala hutaamini kamwe maisha yako;

67asubuhi utasema, Laiti ingekuwa jioni! Na jioni utasema, Laiti ingekuwa asubuhi! Kwa kicho cha moyo wako utakavyokucha, na kuona kwa macho yako utakavyoona.[#Ayu 7:4]

68BWANA atakurudisha tena Misri kwa merikebu, kwa njia ambayo nilikuambia, Hutaiona tena popote; nanyi huko mtajiuza nafsi zenu kwa adui zenu kuwa watumwa na wajakazi, wala hapana atakayewanunua.[#Yer 44:7; Hos 8:13; 9:3]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya