Kumbukumbu la Torati 3

Kumbukumbu la Torati 3

Kushindwa kwa mfalme Ogu

1Ndipo tukageuka, tukakwea njia ya Bashani; na Ogu, mfalme wa Bashani, akatutokea juu yetu, yeye na watu wake wote, kuja kupigana huko Edrei.

2BWANA akaniambia, Usimwogope; kwa kuwa nimemtia mikononi mwako, yeye na watu wake wote na nchi yake; nawe utamtenda kama ulivyomtenda Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni.[#Hes 21:24]

3Basi BWANA, Mungu wetu, akamtia mikononi mwako na Ogu mfalme wa Bashani, na watu wake wote; tukampiga, asibakizwe yeyote.

4Tukatwaa miji yake yote wakati huo; hapakuwa na mji tusiotwaa kwao miji sitini, nchi yote ya Argobu, ndio ufalme wa Ogu ulio katika Bashani.[#Kum 29:8; 1 Fal 4:13]

5Miji hiyo yote ilikuwa yenye maboma marefu, na malango, na makomeo, pamoja na vijiji visivyokuwa na maboma, vingi sana.

6Tukaiharibu kabisa, kama tulivyomfanya huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, kwa kuharibu kabisa kila mji uliokuwa na wanaume, wanawake na watoto.[#Kum 2:24; Zab 135:10-12; 136:19-21]

7Lakini wanyama wote wa mji, na nyara za miji, tulitwaa kuwa mawindo yetu.

8Tukaitwaa na nchi wakati huo, katika mikono ya hao wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ng'ambo ya Yordani, kutoka bonde la Arnoni mpaka kilima cha Hermoni;

9(na hiyo Hermoni Wasidoni huiita Sirioni, na Waamori huiita Seniri);[#Zab 29:6; 89:12; 1 Nya 5:23]

10miji yote ya nchi tambarare, na Gileadi yote, na Bashani yote, mpaka Saleka na Edrei, nayo ni miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani.[#Kum 4:49; Yos 12:5; 13:11]

11(Kwani aliyesalia katika mabaki ya Warefai ni Ogu pekee, mfalme wa Bashani; tazama, kitanda chake kilikuwa kitanda cha chuma; kitanda hicho kingali kiko Raba kwa wana wa Amoni? Urefu wake ulikuwa ni dhiraa tisa, na upana wake dhiraa nane, kwa mfano wa mkono wa mtu).[#Amo 2:9; Mwa 14:5; 2 Sam 12:26; Yer 49:2; Eze 21:20; Amo 1:14; #3:11 Au, sanduku lake la jiwe alimozikwa.]

12Na nchi hiyo tuliitwaa ikawa milki yetu, wakati huo; kutoka Aroeri iliyo kwenye bonde la Arnoni, na nusu ya nchi ya milima ya Gileadi, na miji iliyokuwamo, niliwapa Wareubeni na Wagadi;[#Kum 2:36; Yos 12:2; 13:9-12; 2 Fal 10:33; Hes 32:33-38]

13na nchi ya Gileadi iliyobaki, na Bashani yote, maana huo ufalme wa Ogu niliwapa nusu ya kabila la Manase; nchi yote ya Argobu, nayo ndiyo Bashani yote. (Na nchi hii yaitwa nchi ya Warefai.[#Hes 32:39-42; Yos 13:29; 1 Nya 5:26]

14Yairi, mwana wa Manase, alitwaa nchi yote ya Argobu, hata mpaka wa Wageshuri na Wamaaka; akaziita nchi hizo Hawoth-yairi, kwa jina lake mwenyewe, hata hivi leo, maana, hizo nchi za Bashani.)[#1 Nya 2:22; 2 Sam 3:3; 10:6]

15Na Makiri nilimpa Gileadi.[#Hes 26:29; 32:39; Yos 17:1]

16Na Wareubeni na Wagadi niliwapa tokea Gileadi mpaka bonde la Arnoni, katikati ya bonde, na mpaka wake; mpaka mto wa Yaboki, nao ni mpaka wa wana wa Amoni;[#2 Sam 24:5; Hes 21:24]

17na nchi ya Araba nayo, na mto wa Yordani, na mpaka wake, tokea Kinerethi mpaka bahari ya hiyo Araba, nayo ni Bahari ya Chumvi, chini ya materemko ya Pisga, upande wa mashariki.[#Hes 34:11; Mwa 13:10; 14:3; Yos 12:3]

18Nikawaamuru wakati huo, nikawaambia, BWANA, Mungu wenu, amewapa ninyi nchi hii muimiliki, basi vukeni ng'ambo wenye silaha mbele ya ndugu zenu, wana wa Israeli, nyote mlio mashujaa.[#Yos 1:12-15]

19Lakini wake wenu na watoto wenu, na wanyama wenu wa mji, (nawajua kwamba mna wanyama wengi), na wakae katika miji yenu niliyowapa;

20hata BWANA awapumzishe ndugu zenu kama ninyi, nao pia waimiliki nchi wapewayo na BWANA, Mungu wenu, ng'ambo ya Yordani; ndipo mtakaporudi kila mmoja aende katika milki yake niliyowapa.[#Yos 22:4]

21Nikamwamuru Yoshua wakati huo, nikamwambia, Macho yako yameona yote aliyowatenda BWANA, Mungu wenu, wale wafalme wawili, navyo ndivyo atakavyoutenda BWANA kila ufalme huko uvukiako.

22Msiwache, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye awapiganiaye.[#Kut 14:14; Kum 1:30; 20:4]

Musa aitazama Kanaani kutoka Pisga

23Nikamnyenyekea BWANA wakati huo, nikamwambia,[#Hes 27:12-14; Kum 32:48-52]

24Ee BWANA Mungu, umeanza kumwonesha mtumishi wako ukubwa wako, na mkono wako wa nguvu; kwani kuna mungu gani mbinguni au duniani awezaye kufanya mfano wa kazi zako, na mfano wa matendo yako yenye nguvu?[#Kum 11:2; Neh 9:32; Zab 106:2; 145:3,6; Yer 32:18-21; Kut 15:11; 2 Sam 7:22; Zab 71:19; 86:8]

25Nami nakuomba nivuke, nikaione hiyo nchi nzuri iliyoko ng'ambo ya Yordani, mlima ule mzuri, na Lebanoni.[#Kut 3:8; Kum 4:22]

26Lakini BWANA alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize; BWANA akaniambia, Na ikutoshe, usinene nami zaidi jambo hili.

27Kwea katika kilele cha Pisga ukainue macho yako upande wa magharibi, na kaskazini, na kusini, na mashariki, ukatazame kwa macho yako, kwa maana huuvuki mto huu wa Yordani.

28Lakini mwagize Yoshua, mtie moyo na nguvu, umtie na nguvu; kwani ndiye atakayevuka mbele ya watu hawa, na nchi utakayoiona atawarithisha yeye.[#Hes 27:18; Kum 1:38; 31:3,7]

29Basi tukakaa katika bonde lililoelekea Beth-peori.[#Kum 4:46]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya