The chat will start when you send the first message.
1Musa akapanda kutoka uwanda wa Moabu mpaka mlima Nebo, hata kilele cha Pisga kukabili Yeriko. BWANA akamwonesha nchi yote ya Gileadi hata Dani;[#Yos 19:40-48; Amu 18:28]
2na Naftali yote, na nchi ya Efraimu na Manase, na nchi yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi;[#Kut 23:31; Hes 34:6; Kum 11:24; Yos 15:12]
3na Negebu, na uwanja wa bonde la Yeriko, mji wa mitende, hata mpaka Soari.[#Amu 1:16; 3:13; 2 Nya 28:15]
4BWANA akamwambia, Hii ndiyo nchi niliyowaapia Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, nikisema, Nitawapa wazao wako. Basi nimekuonesha kwa macho yako, lakini hutavuka huko.[#Mwa 12:7; 26:3; 28:13]
5Basi Musa, mtumishi wa BWANA, akafa huko, katika nchi ya Moabu, kwa neno la BWANA.[#Kum 32:50; Yos 1:1,2; Mal 4:4]
6Akamzika bondeni, katika nchi ya Moabu, kukabili Beth-peori; lakini hapana mtu ajuaye kaburi lake hata leo.[#Yud 1:9]
7Musa alikuwa mtu wa miaka mia moja na ishirini alipokufa; jicho lake halikupofuka, wala nguvu za mwili wake hazikupunguka.[#Kum 31:2; Mwa 27:1; 48:10; Yos 14:10]
8Wana wa Israeli wakamwombolezea Musa katika uwanda wa Moabu siku thelathini; basi siku za maombolezo ya matanga ya Musa zikaisha.[#Mwa 50:3; Hes 20:29; 1 Sam 25:1; Isa 57:1; Mdo 8:2]
9Na Yoshua, mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama BWANA alivyomwamuru Musa.[#Kut 31:3; Hes 11:17; 1 Fal 9:12; Isa 11:2; Dan 6:3; Hes 27:18]
10Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye BWANA alimjua uso kwa uso;[#Kut 33:11; Kum 18:15,18; Hes 12:6; Kum 5:4]
11katika ishara zote na maajabu yote, ambayo BWANA alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote;
12na katika ule mkono wa nguvu wote, tena katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote.