The chat will start when you send the first message.
1Amri hii ninayokuamuru leo mtaizingatia, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo BWANA aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki.
2Nawe utaikumbuka njia ile yote BWANA, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arubaini katika jangwa, ili akunyenyekeze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo.[#Zab 136:16; Amo 2:10; 2 Nya 32:31; Yn 2:25]
3Akakunyenyekeza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha BWANA.[#Mt 4:4; Lk 4:4; Kut 16:2; Zab 78:23-25; 105:40,41; 1 Kor 10:3,4; Zab 104:29; Lk 12:29-31; Ebr 13:5,6]
4Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arubaini.[#Kum 29:5; Neh 9:21]
5Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo BWANA, Mungu wako, akurudivyo.[#2 Sam 7:14; Zab 89:32; Mit 3:12; Ebr 12:5; Ufu 3:19]
6Nawe uzishike amri za BWANA, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha.
7Kwa kuwa BWANA, Mungu wako, anakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima;
8nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali;
9nchi utakayokula mikate humo, pasina shida, hutapungukiwa na kitu ndani yake; nchi ambayo mawe yake ni chuma, na milima yake mnaweza kuchimba shamba.
10Nawe utakula ushibe, utamshukuru BWANA, Mungu wako, kwa nchi nzuri aliyokupa.[#Zab 103:2; 1 Kor 10:31; 1 The 5:18; 1 Tim 4:3]
11Jihadhari, usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo.[#Hos 13:5-6]
12Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake;[#Mit 30:9; Hos 13:6]
13na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka;
14basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa;[#1 Kor 4:7; Zab 106:21]
15aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu,[#Isa 63:12; Yer 2:6; Hes 21:6; Hos 13:5; Hes 20:11]
16aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako.[#Kut 16:15; Rum 8:28; 2 Kor 4:17; Ebr 12:11; Yak 1:12; 1 Pet 1:7]
17Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo.[#Kum 9:4; 1 Kor 4:7]
18Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.[#Mit 10:22; Hos 2:8]
19Lakini itakuwa, kama ukimsahau BWANA, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawaonya leo ya kuwa mtaangamia bila shaka.
20Kama vile mataifa yale ambayo BWANA anawaangamiza mbele yenu, ndivyo mtakavyoangamia; kwa sababu hamkutaka kuisikiliza sauti ya BWANA, Mungu wenu.[#Omb 1:1-22; 2:17; Eze 5:5-17; Dan 9:12; Zek 1:6]