The chat will start when you send the first message.
1Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu walioko [Efeso] wanaomwamini Kristo Yesu.[#Mdo 18:19-21; 19:1; Rum 1:7; Kol 1:1; 1 Kor 1:2]
2Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.[#Kol 1:2]
3Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;[#Efe 2:6]
4kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.[#Yn 15:16; 17:24; Efe 5:27; Rum 8:29]
5Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, kulingana na radhi ya mapenzi yake.[#Yn 1:12]
6Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.[#Mt 3:17; Kol 1:13]
7Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.[#Kol 1:14,20; Efe 2:7; 3:8,16]
8Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi;[#Kol 1:9]
9akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, kulingana na radhi yake aliyoikusudia katika yeye huyo.[#Efe 3:9; Rum 16:25]
10Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo;[#Gal 4:4; Kol 1:16]
11na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake.[#Kol 1:12; Rum 8:28]
12Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu.
13Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, Habari Njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa mhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.[#Efe 4:30; Kol 1:5,6]
14Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.[#2 Kor 1:22; 5:5]
15Kwa sababu hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote,[#Kol 1:4,9]
16siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu,[#Kol 1:3]
17Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;[#Kol 1:10]
18macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;[#Kum 33:3,4; Efe 4:4; Kol 1:5,11]
19na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake;[#2 Kor 13:4; Kol 1:11; 2:12]
20aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka katika mkono wake wa kulia katika ulimwengu wa roho;[#Zab 110:1]
21juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na utawala, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;[#Kol 1:16; 2:10]
22akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo[#Zab 8:6; Mt 28:18; Efe 4:15; Kol 1:18]
23ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.[#Rum 12:5; Kol 1:19; 1 Kor 12:27; Efe 4:10]