The chat will start when you send the first message.
1Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;[#Kol 1:21; 2:13]
2ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;[#Efe 6:12; Tit 3:3; Yn 12:31; Kol 1:13]
3ambao zamani, sisi sote nasi tulienda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira, kama wengineo wote.[#Kol 3:6]
4Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda;
5hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alitufanya kuwa hai pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema.[#Lk 15:24,32; Efe 5:14; Rum 6:13]
6Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;[#Rum 8:10; Flp 3:20]
7ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu.[#Efe 1:7]
8Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;[#Gal 2:16]
9wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.[#1 Kor 1:29]
10Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.[#Tit 2:14]
11Kwa ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara ya mwilini iliyofanyika kwa mikono;[#Efe 5:8]
12kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani.[#Rum 9:4; 1 The 4:13]
13Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.[#Isa 57:19; 52:7; Kol 1:20]
14Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga.[#Isa 9:5; Gal 3:28; Kol 2:14]
15Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani.[#Kol 2:14; 2 Kor 5:17]
16Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuumaliza ule uadui kwa huo msalaba.[#Kol 1:20,22]
17Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu.[#Isa 57:19; Zek 9:10]
18Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.[#Efe 3:12]
19Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu.[#Efe 3:6; Ebr 12:22,23]
20Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.[#Mt 16:18; Isa 28:16]
21Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana.[#Kol 2:19]
22Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.[#1 Pet 2:5]