Waefeso 6

Waefeso 6

Watoto na wazazi

1Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.[#Kol 3:20]

2Waheshimu baba yako na mama yako; hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,[#Kut 20:12; Kum 5:16]

3Upate heri na kuishi siku nyingi katika dunia.

4Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maagizo ya Bwana.[#Kol 3:21; Isa 50:5; Mit 2:2; 3:11; 19:18; Kum 6:7,20-25; Zab 78:4]

Watumwa na mabwana

5Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba mnamtii Kristo;[#Kol 3:22-25; Tit 2:9,10; 1 Pet 2:18]

6wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekazao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo;

7kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu;

8mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana awe ni mtumwa au ni mtu huru.[#2 Kor 5:10]

9Nanyi, mabwana, watendeeni wao yayo hayo, pasipo kuwatisha, huku mkijua ya kuwa yeye aliye Bwana wao na wenu yuko mbinguni, wala kwake hakuna upendeleo.[#Kum 10:17; Kol 3:25; 4:1; 2 Nya 19:7; Mdo 10:34]

Silaha zote za Mungu

10Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.[#1 Kor 16:13; 1 Yoh 2:14]

11Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.[#Efe 4:14; 2 Kor 10:4]

12Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.[#Efe 2:2; Yn 14:30; Kol 1:13; 1 Pet 5:8,9]

13Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.[#1 Fal 20:11]

14Basi simameni, mkiwa mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,[#Isa 11:5; 59:17; Lk 12:35; 1 Pet 1:13; 1 The 5:8]

15na kama viatu vilivyofungiwa miguuni mwenu muwe tayari kutangaza Injili ya amani;[#Isa 52:7; 40:3,9]

16zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.[#1 Pet 5:9; 1 Yoh 5:4]

17Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;[#Isa 59:17; 11:4; 49:2; 51:16; 1 The 5:8; Hos 6:5]

18kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;[#Mt 26:41; Kol 4:2,3]

19pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili;[#Kol 4:3; 2 The 3:1; Mdo 4:29]

20ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.[#2 Kor 5:20; Kol 4:4]

Mambo ya binafsi na baraka

21Basi ili nanyi pia mpate kuzijua habari zangu, ni hali gani, Tikiko, ndugu mpendwa, mhudumu mwaminifu katika Bwana, atawajulisheni mambo yote;[#Mdo 20:4; 2 Tim 4:12; Kol 4:7; #Kol 4:7-8]

22ambaye ninamtuma kwenu kwa kusudi lilo hilo mpate kuzijua habari zetu, naye awafariji mioyo yenu.[#Kol 4:7,8]

23Amani na iwe kwa ndugu, na upendo, pamoja na imani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo.

24Neema na iwe pamoja na wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo kwa upendo usioisha.[#1 Pet 1:8]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya