The chat will start when you send the first message.
1Hata ulipofika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku yake ya kumi na tatu, amri ya mfalme na mbiu yake ilipowadia kutekelezwa; ambayo siku ile adui za Wayahudi walitumaini kuwatawala, bali kumebadilika kinyume, hata Wayahudi waliwatawala wale waliowachukia;[#Est 8:12; 3:13; 2 Sam 22:41; Isa 14:2]
2siku ile ile Wayahudi wakakusanyika mijini mwao katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero ili kuwatia mikono wale watu waliowatakia hasara; wala asiweze mtu kuwazuia, kwa kuwa waogopwa na watu wote.
3Nao wakuu wa mikoa, na majumbe, na watawala, na wale waliofanya shughuli ya mfalme, waliwasaidia Wayahudi; maana walimwogopa Mordekai.
4Maana Mordekai alikuwa mkuu nyumbani mwa mfalme, na sifa yake imevuma katika mikoa yote, kwa kuwa huyo Mordekai amezidi kukuzwa.
5Basi Wayahudi wakawapiga adui zao wote mapigo ya upanga, na kuwachinja, na kuwaangamiza, wakawatenda kama wapendavyo wale waliowachukia.
6Hata huko Susa mjini Wayahudi wakawaua watu mia tano, na kuwaangamiza.
7Wakawaua na Parshandatha, na Dalfoni, na Aspatha,
8na Poratha, na Adalia, na Aridatha,
9na Parmashta, na Arisai, na Aridai, na Waizatha,
10wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui ya Wayahudi; lakini juu ya nyara hawakuweka mikono.
11Siku ile mfalme akaletewa hesabu ya hao waliouawa huko Susa mjini.
12Mfalme akamwambia malkia Esta, Wayahudi wamewaua watu mia tano hapa Shushani ngomeni na kuwaangamiza, pamoja na wana kumi wa Hamani, je! Wamefanyaje basi katika majimbo ya mfalme yaliyosalia! Basi, una nini uombalo? Nawe utapewa; ama unayo haja gani tena? Nayo itatimizwa.
13Ndipo Esta aliposema, Mfalme akiona vema, Wayahudi walioko Susa na wapewe ruhusa kufanya tena kesho sawasawa na mbiu ya leo, na hao wana kumi wa Hamani watundikwe juu ya mti ule.
14Mfalme akaamuru ifanyike vivyo hivyo, mbiu ikapigwa huko Susa, wakawatundika wale wana kumi wa Hamani.
15Basi Wayahudi wa Susa wakakusanyika tena siku ya kumi na nne pia ya mwezi wa Adari, wakawaua watu mia tatu huko Susa; lakini juu ya nyara hawakuweka mikono.
16Nao Wayahudi wengine waliokaa katika mikoa ya mfalme walikusanyika, wakayapigania maisha yao, wakajipatia raha mbele ya adui zao, wakawaua waliowachukia, watu elfu sabini na tano; lakini juu ya nyara hawakuweka mikono.
17Hii ndiyo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari; na siku ya kumi na nne ya mwezi huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha.
18Lakini Wayahudi wa Susa walikusanyika siku ya kumi na tatu ya mwezi huo, na siku ya kumi na nne pia; na siku ya kumi na tano ya mwezi uo huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha.
19Kwa sababu hii Wayahudi wa vijijini, wakaao katika miji isiyo na ngome, huishika siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, kuwa siku ya furaha na karamu, sikukuu ya kupelekeana zawadi.
20Basi Mordekai aliyaandika mambo hayo; naye akatuma barua kwa Wayahudi wote waliokaa katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero, waliokuwa karibu na waliokuwa mbali,
21kuwaonya wazishike siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, na siku ya kumi na tano yake, kila mwaka,
22siku ambazo Wayahudi walijipatia raha mbele ya adui zao, na mwezi uliogeuzwa kwao kuwa furaha badala ya huzuni, na kuwa sikukuu badala ya kilio; wazifanye siku hizo ziwe za karamu na furaha, za kupeana zawadi na za kuwapa maskini tunu.
23Nao Wayahudi wakakubali kufanya kama walivyoanza, na kama Mordekai alivyowaandikia;
24kwa sababu Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi wote, alikuwa amefanya shauri juu ya Wayahudi ili kuwaangamiza, akapiga Puri, yaani kura, ili kuwakomesha na kuwaangamiza pia;[#Est 3:6]
25bali mfalme alipoarifiwa, aliamuru kwa barua ya kwamba huo mpango mwovu alioufanya juu ya Wayahudi umrudie kichwani pake mwenyewe; na ya kwamba yeye na wanawe watundikwe juu ya mti.
26Hivyo wakaziita siku hizo Purimu, kwa jina la Puri. Basi, kwa ajili ya maneno yote ya barua hiyo, na kwa yale waliyoyaona wenyewe juu ya jambo hilo, na mambo yenyewe yaliyowapata,
27Wayahudi wakaagiza na kuweka wajibu juu yao wenyewe, na juu ya wazao wao, na juu ya wote watakaojiunga nao, isikome, ya kwamba watazishika siku hizo mbili kulingana na andiko lile, na kwa majira yake kila mwaka;
28siku hizo zikumbukwe na kushikwa kwa vizazi vyote na kila jamaa, katika kila jimbo na kila mji; wala siku hizo za Purimu zisikome katikati ya Wayahudi, wala kumbukumbu lake lisiishe kwa wazao wao.
29Ndipo malkia Esta, binti Abihaili, pamoja na Mordekai Myahudi, alipoandika kwa mamlaka yote kuithibitisha barua hii ya pili ya Purimu.
30Akapeleka barua kwa Wayahudi wote katika majimbo yote mia na ishirini na saba ya ufalme wake Ahasuero, maneno ya amani na kweli,
31ili kuzithibitisha siku hizo za Purimu kwa majira yake, kama Mordekai Myahudi na malkia Esta walivyoamuru, na kama walivyojiagizia juu yao wenyewe, na juu ya wazawa wao, kwa kufunga na kulia.
32Amri yake Esta ikayathibitisha mambo hayo ya Purimu; ikaandikwa katika kitabu.