Kutoka 21

Kutoka 21

Sheria kuhusu watumwa

1Basi hukumu utakazoziweka mbele ya watu ni hizi[#Kut 24:3; Kum 4:14; 6:1]

2Ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako huru bure.[#Law 25:39-46; Kum 15:12; Yer 34:14]

3Ikiwa aliingia kwako peke yake tu, atatoka hivyo peke yake; kama ameoa, mkewe atatoka aende pamoja naye.

4Ikiwa ni bwana wake aliyemwoza huyo mke, naye amemzalia wana, wa kiume au wa kike; yule mke na wanawe watakuwa ni mali ya bwana wake, naye mume atatoka peke yake.[#Law 25:44]

5Lakini huyo mtumwa akisema waziwazi, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; sitaki mimi kutoka niwe huru;[#Kum 15:16]

6ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake atalitoboa sikio lake kwa uma; ndipo atamtumikia sikuzote.[#Kut 12:12; 22:8; Kum 16:18; Zab 82:1; 40:6]

7Mtu akimwuza binti yake awe kijakazi, hatatoka yeye kama watumwa wa kiume watokavyo.[#Neh 5:5]

8Ikiwa bwana wake hakupendezewa naye, akiwa amemposa, ndipo atakubali akombolewe; hana amri yeye kumwuza aende kwa watu wageni maana amemtenda kwa udanganyifu.

9Akimposa mwanawe, atamtendea kama desturi zipasazo binti zake.

10Akijitwalia mke mwingine, chakula chake huyo, na nguo zake, na ngono yake, hatampunguzia.[#1 Kor 7:5]

11Ikiwa hamfanyii mambo haya matatu, ndipo atatoka aende bure, pasipo kutolewa mali.

Sheria kuhusu uhalifu

12Mtu yeyote ampigaye mtu, hata akafa, hana budi atauawa huyo.[#Law 24:17; Mwa 9:6; Hes 35:30; Mt 26:52]

13Lakini kama hakumvizia, ila Mungu amemtia mkononi mwake; basi nitakuonesha mahali atakapopakimbilia.[#Hes 35:10-34; Kum 19:1-13; Yos 20:1-9; 1 Sam 24:4,10,18]

14Lakini, mtu akimwendea mwenziwe kwa kujikinai, kusudi apate kumwua kwa hila; huyo utamwondoa hata madhabahuni pangu, auawe.[#Hes 15:30; Kum 19:11; Ebr 10:26; 1 Fal 2:28-34; 2 Fal 11:15]

15Ampigaye baba yake au mama yake, sharti atauawa.

16Yeye amwibaye mtu, na kumwuza, au akipatikana mkononi mwake, sharti atauawa huyo.[#Kum 24:7; Mwa 37:28; Kut 22:4]

17Yeye amwapizaye baba yake au mama yake, sharti atauawa.[#Law 20:9; Mt 15:4; Mk 7:10; Mit 20:20]

18Watu wakigombana, na mmoja akimpiga mwenziwe kwa jiwe, au kwa konde, asife, lakini yualazwa kitandani mwake;

19atakapoinuka tena na kuenenda nje kwa kutegemea fimbo, ndipo hapo yule aliyempiga ataachwa; ila atamlipa kwa ajili ya hayo majira yake yaliyompotea, naye atamwuguza hata apone kabisa.[#2 Sam 3:29]

20Mtu akimpiga mtumwa wake, au kijakazi chake, kwa fimbo, naye akifa mkononi mwake, hana budi ataadhibiwa.[#Law 25:43; Efe 6:9]

21Lakini akipona siku moja au mbili hataadhibiwa; maana, ni mali yake.[#Law 25:45]

22Watu wanaume wakipigana, wakamwumiza mwanamke mwenye mimba hata akaharibu mimba, tena yasiwe madhara zaidi; sharti atatozwa mali kama atakavyomwandikia mumewe huyo mwanamke; atalipa kama hao waamuzi watakavyosema.[#Kum 22:18,19]

23Lakini kwamba pana madhara zaidi, ndipo utatoza uhai kwa uhai,

24jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu,[#Law 24:19-20; Kum 19:21; Mt 5:38; 7:2]

25kuteketeza kwa kuteketeza, jeraha kwa jeraha, chubuko kwa ajili ya chubuko.

26Mtu akimpiga mtumwa wake jicho, au jicho la kijakazi chake, na kuliharibu; atamwacha huru kwa ajili ya jicho lake.[#Kol 4:1]

27Au akimpiga mtumwa wake jino likang'oka, au jino la kijakazi chake, atamwacha huru kwa ajili ya jino lake.

Sheria kuhusu mali

28Ng'ombe akimpiga pembe mwanamume au mwanamke, nao wakafa, huyo ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, nyama yake isiliwe; lakini mwenye huyo ng'ombe ataachiliwa.[#Mwa 9:5]

29Lakini kama huyo ng'ombe alizoea kupiga watu tangu hapo, naye mwenyewe ameoneshwa jambo hilo, wala asimzuie, naye amemwua mwanamume au mwanamke; huyo ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, na huyo mwenyewe naye atauawa.

30Lakini akiandikiwa ukombozi, ndipo atakapotoa kwa ajili ya uhai wake hicho atakachoandikiwa.[#Hes 35:31]

31Akiwa ng'ombe amempiga pembe mtoto wa kiume na kumtumbua, au akiwa amempiga mtoto wa kike, atatendwa kama hukumu hiyo.

32Ng'ombe akimtumbua mtumwa mume au kijakazi; mwenye ng'ombe atampa bwana wao shekeli thelathini za fedha, naye ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe.[#Zek 11:12,13; Mt 26:15; Flp 2:7]

33Ikiwa mtu atafunua shimo, au kuchimba shimo, naye asilifunike, kisha ikawa ng'ombe au punda kutumbukia humo,

34mwenye shimo atalipa; atampa huyo mwenye mnyama fedha, na mnyama aliyekufa atakuwa ni wake.

35Ng'ombe wa mtu akimwumiza ng'ombe wa mtu mwingine hata akafa; ndipo watamwuza huyo ng'ombe aliye hai na kugawanya thamani yake; na ng'ombe aliyekufa pia watamgawanya.

36Au ikiwa ilijulikana ya kuwa ng'ombe tangu hapo amezoea kupiga kwa pembe, wala mwenyewe asimzuie; ndipo atakapolipa yeye, ng'ombe kwa ng'ombe, na huyo ng'ombe aliyekufa atakuwa ni wake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya