Kutoka 3

Kutoka 3

Mungu amtokea Musa

1Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu.[#1 Fal 19:8]

2Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kichaka; akatazama, na kumbe! Kile kichaka kiliwaka moto, nacho kichaka hakikuteketea.[#Mdo 7:30-34; Kum 33:16; Isa 63:9]

3Musa akasema, Nitageuka sasa niende nione kioja hiki, kwa nini kichaka hiki hakiteketei.[#Zab 111:2]

4BWANA alipoona ya kuwa ameenda ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kichaka, akasema, Musa! Musa! Akaitika, Mimi hapa.[#Kum 33:16]

5Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni mahali patakatifu.[#Yos 5:15]

6Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akafunika uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu.[#Mwa 28:13; Mk 12:26; Isa 6:1,5; Ufu 1:17]

7BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao;[#Mwa 18:21]

8nami nimeshuka ili niwaokoe kutoka kwa mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hadi nchi njema, kisha pana; nchi itiririkayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.[#Mwa 11:5; Kut 12:51; Kum 1:25; Hes 13:27]

9Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.[#Kut 1:11]

10Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.[#Zab 105:26; Mik 6:4]

11Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri?[#1 Sam 18:18; 1 Fal 3:7-9; Isa 6:5,8; Yer 1:6]

12Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.[#Mwa 31:3; Kum 31:23; Yos 1:5; Isa 43:2; Rum 8:31]

Mungu afunua jina lake takatifu

13Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake ni nani? Niwaambie nini?[#Kut 6:2-3; Mwa 32:29]

14Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu.[#Ufu 1:4,8; Kut 6:3; Yn 8:58; Ebr 13:8; #3:14 Au, Nitakuwa kama Nitakavyokuwa; au, Ndimi Ndiye.; #3:14 Au, Nitakuwa; au, Ndimi.]

15Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.[#Zab 135:13; Hos 12:5; #3:15 Neno hili BWANA au MUNGU lionekanapo kuandikwa kwa herufi kubwa, laonesha jina takatifu sana la Mwenyezi Mungu. Katika Kiebrania huwa YHWH (latamkwa Yahweh). Katika Lugha ya Kiebrania neno YHWH laasilika kwa kiarifa ‘hayah’ ambalo tafsiri yake ni ‘kuwa’]

16Nenda, ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri;[#Mwa 48:15; 50:24; Kut 2:25; 4:31; Kum 26:7; Zab 80:14; Lk 1:68]

17Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka katika mateso ya Misri na kuwaingiza katika nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali.[#Mwa 15:14]

18Nao watakusikia sauti yako; nawe utakwenda, wewe na wazee wa Israeli kwa mfalme wa Misri, na kumwambia, BWANA Mungu wa Waebrania, amekutana nasi; basi sasa twakuomba, tupe ruhusa twende mwendo wa siku tatu jangwani, ili tumtolee dhabihu BWANA Mungu wetu.[#Hes 23:3]

19Nami najua ya kuwa huyo mfalme wa Misri hatawapa ruhusa mwende zenu, la, hata kwa mkono wa nguvu.

20Nami nitaunyosha mkono wangu, na kuipiga Misri kwa ajabu zangu zote, nitakazofanya kati yake, kisha baadaye atawapa ruhusa kwenda.[#Kut 7:3; 12:31; Kum 6:22; Neh 9:10; Zab 105:27; 135:9; Yer 32:20; Mdo 7:36]

21Nami nitawapa watu hao kufadhiliwa mbele ya Wamisri; hata itakuwa, hapo mtakapokwenda zenu hamtakwenda kitupu;[#Kut 11:3; 12:35-36; Zab 106:46; Mit 16:7]

22Lakini kila mwanamke ataomba kwa jirani, na kwa huyo akaaye naye nyumbani, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi; nanyi mtawavika wana wenu na binti zenu; nanyi mtawateka nyara Wamisri.[#Mwa 15:14; Kut 11:2; Ayu 27:17; Mit 13:22; Eze 39:10]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya