The chat will start when you send the first message.
1Na zile nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, wakafanya mavazi yaliyofumwa kwa ustadi sana kwa ajili ya kutumika katika mahali patakatifu, na kuyatengeneza hayo mavazi matakatifu ya Haruni, vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.[#Kut 35:23; 31:10; 35:19; Zab 93:5; Eze 43:12; Kut 28:4]
2Naye akaifanya hiyo naivera, ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya buluu, zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa.[#Kut 28:6; Law 8:7]
3Nao wakaifua hiyo dhahabu hata ikawa mabamba membamba sana, kisha wakaikata iwe nyuzi, ili wapate kuifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyuzi nyekundu na za kitani nzuri, kazi ya fundi stadi sana.
4Nao wakafanya na vipande vya mabegani kwa ajili yake, vilivyoungwa pamoja; viliungwa pamoja kwa ncha zake mbili.
5Na huo mshipi wa kazi ya werevu, uliokuwa juu yake ili kuifunga mahali pake; ulikuwa wa kitu kimoja, na wa kazi moja na naivera ya dhahabu, na rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.[#Isa 11:5; Ufu 1:13]
6Nao wakavitengeza vile vito vya shohamu, vilivyotiwa katika vijalizo vya dhahabu, vilivyochorwa mfano wa kuchora kwake mhuri, kwa majina ya hao wana wa Israeli.[#Kut 28:9; Ayu 28:16; Isa 49:16; Ufu 2:17]
7Naye akavitia katika vile vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli, kama BWANA alivyomwagiza Musa.[#Kut 28:12; Yos 4:7; Neh 2:20]
8Naye akafanya kile kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi, kama hiyo kazi ya naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa.[#Kut 28:15; Isa 59:17]
9Kilikuwa mraba; wakakifanya kile kifuko cha kifuani kwa kukikunja; urefu wake ulikuwa shibiri, na upana wake ulikuwa shibiri, tena kilikuwa ni cha kukunjwa.
10Nao wakatia safu nne za vito ndani yake, safu moja ilikuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, vilikuwa ni safu ya kwanza.[#Kut 28:17; Eze 28:13; Ufu 21:19,20; Isa 54:12]
11Na safu ya pili ilikuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi.[#Ufu 4:3; Isa 54:11; Yer 17:1]
12Na safu ya tatu ilikuwa ni hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto.
13Na safu ya nne ilikuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi: vito hivyo vilikuwa vimetiwa katika vijalizo vya dhahabu, kila kimoja mahali pake.[#Dan 10:6; Ayu 28:16; Ufu 21:11]
14Na hivyo vito vilikuwa vyaandama majina ya wana wa Israeli, kumi na mawili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora mihuri, kila moja kwa jina lake, kwa yale makabila kumi na mawili.
15Nao wakafanya katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa ya dhahabu safi.
16Nao wakafanya vijalizo viwili vya dhahabu, na pete mbili za dhahabu; nao wakazitia hizo pete mbili katika ncha mbili za hicho kifuko.
17Nao wakaitia hiyo mikufu miwili iliyosokotwa katika hizo pete mbili zilizokuwa katika ncha mbili za hicho kifuko.
18Na ncha hizo mbili nyingine, za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa, wakazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera, upande wa mbele.
19Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani.
20Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi.
21Nao wakakikaza kile kifuko kwa pete zake kwenye naivera kwa ukanda wa rangi ya samawati, ili kikae pale juu ya mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, na ya kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.
22Naye akafanya hilo joho la naivera ya kazi ya kusuka, rangi ya samawati yote;[#Kut 28:31; Law 8:7; 1 Sam 2:18; 2 Sam 6:14]
23na hilo tundu lililokuwa katikati yake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, na utepe wake kulizunguka hilo tundu, ili lisipasuke.
24Nao wakatia katika upindo wa joho makomamanga ya nyuzi za rangi ya samawati, na rangi ya zambarau, na rangi nyekundu, na kitani iliyosokotwa.
25Nao wakafanya njuga za dhahabu safi, na kuzitia hizo njuga kati ya hayo makomamanga pande zote, kati ya hayo makomamanga;[#Kut 28:33]
26njuga na komamanga, njuga na komamanga katika pindo za joho kuizunguka pande zote, ili kutumika kwa hiyo; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.
27Nao wakafanya hizo kanzu za nguo ya kitani nzuri ya kufumwa, kwa Haruni, na kwa wanawe[#Kut 28:39,40; 39:27; Law 8:13; Kut 28:4; Isa 61:10; Rum 3:22; Gal 3:27]
28na hicho kilemba cha nguo ya kitani nzuri, na zile kofia nzuri za kitani, na hizo suruali za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa,[#Kut 28:39,42; Law 6:10; 16:4; Eze 44:17,18]
29na huo mshipi wa nguo nzuri ya kitani iliyosokotwa, na rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, kazi ya fundi mwenye kutia taraza; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.
30Nao wakafanya hilo bamba la hilo taji takatifu la dhahabu safi, na kuandika juu yake andiko, mfano wa kuchorwa kwa mhuri, MTAKATIFU KWA BWANA.[#Zab 93:5; Zek 14:20; Isa 23:18]
31Nao wakatia ukanda wa rangi ya samawati ili kulifunga katika hicho kilemba upande wa juu; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.
32Basi ndivyo ilivyomalizwa kazi yote ya maskani ya hema ya kukutania; na wana wa Israeli walifanya kama yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya.[#Kut 25:40]
33Nao wakamletea Musa hiyo maskani; yaani Hema, na vyombo vyake vyote, vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na nguzo zake, na vitako yake;[#Ebr 9:1-28]
34na kifuniko chake cha ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na kifuniko cha ngozi za pomboo, na pazia la sitara;
35na sanduku la ushuhuda, na miti yake, na kiti cha rehema;
36na meza, na vyombo vyake vyote, na mikate ya wonyesho;
37na kinara cha taa safi, na taa zake, hizo taa za kuwekwa mahali pake, na vyombo vyake vyote, na mafuta ya taa,[#Ufu 1:13-20; Kut 27:21; Mt 5:14; Flp 2:15]
38na madhabahu ya dhahabu, na mafuta ya kutiwa, na uvumba mzuri, na pazia kwa mlango wa hema;
39na madhabahu ya shaba, na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na birika na kitako chake;[#Kut 38:30; 1 Fal 8:64]
40na ukuta wa nguo wa ua, na nguzo zake na vitako vyake, na pazia la lango la ua, na kamba zake, na vigingi vyake, na vyombo vyote vya kutumiwa katika utumishi wa maskani, kwa hiyo hema ya kukutania,[#Ufu 3:12]
41na mavazi ya kazi nzuri kwa utumishi katika mahali patakatifu, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
42Sawasawa na yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyoifanya hiyo kazi yote wana wa Israeli.[#Kut 35:10]
43Musa akaiona hiyo kazi yote, na tazama, walikuwa wameimaliza; vile vile kama BWANA alivyoagiza, walikuwa wameifanya vivyo hivyo; basi Musa akawaombea heri.[#Mwa 14:19; Law 9:22; Hes 6:23; Yos 22:6; 2 Sam 6:18; 1 Fal 8:14; 2 Nya 30:27]