Ezekieli 14

Ezekieli 14

Hukumu za Mungu zathibitishwa

1Ndipo baadhi ya wazee wa Israeli wakanijia, wakaketi mbele yangu.[#Eze 8:1; 20:1]

2Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema,

3Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Nitakubali kuombwa ushauri na wao?[#Eze 3:20; 7:19; 1 Pet 2:8; Ufu 2:14; Mit 15:8]

4Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, BWANA, nitamjibu neno lake kulingana na wingi wa sanamu zake;

5ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao.[#Ebr 3:12-19]

6Kwa sababu hiyo uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu; mkageuze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote.

7Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, kisha kumwendea nabii, na kuniuliza neno kwa ajili ya nafsi yake; mimi, BWANA, nitamjibu, mimi mwenyewe;[#Yer 2:13; Mt 6:24; Yud 1:19]

8nami nitaukaza uso wangu juu ya mtu yule, na kumfanya kuwa ajabu, awe ishara na mithali, nami nitamkatilia mbali, asiwe kati ya watu wangu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.[#Law 17:10; Yer 44:11; Eze 15:7; 5:15; Hes 26:10; Kum 28:37]

9Na nabii akidanganyika, na kusema neno, mimi, BWANA, nimemdanganya nabii yule, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli.[#Ayu 12:16; Yer 4:10; 2 The 2:11]

10Nao watauchukua uovu wao; uovu wa nabii utakuwa sawasawa na uovu wake yule amwendeaye aulize neno;

11ili nyumba ya Israeli wasipotee mbali nami, wala wasijitie unajisi tena kwa makosa yao yote; bali wawe watu wangu, nami niwe Mungu wao, asema Bwana MUNGU.[#Zab 119:67,71; Ebr 12:11; Yer 31:18,19; 2 Pet 2:15; Yer 24:7; 30:22; 32:38; Eze 11:20; 36:28]

12Neno la BWANA likanijia, kusema,

13Mwanadamu, nchi itakapofanya dhambi na kuniasi, kwa kukosa, nikaunyosha mkono wangu juu yake, na kulivunja tegemeo la chakula chake, na kuiletea njaa, na kukatilia mbali mwanadamu na mnyama;[#Law 26:26; Isa 3:1; Eze 4:16]

14wajapokuwa watu hawa watatu, Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kuwamo ndani yake, wangejiokoa nafsi zao wenyewe tu kwa haki yao, asema Bwana MUNGU.[#Yer 15:1; 7:16; Mit 11:4; 2 Pet 2:9]

15Nikipitisha wanyama wabaya ndani ya nchi ile, wakaiharibu hata ikawa ukiwa, mtu awaye yote asiweze kupita ndani yake, kwa sababu ya wanyama hao;[#Hes 21:6; Law 26:22]

16wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; wao wenyewe tu wataokoka, bali nchi ile itakuwa ukiwa.

17Au nikileta upanga juu ya nchi ile, na kusema, Upanga, pita kati ya nchi hii, hata nikawakatilia mbali na nchi hiyo wanadamu na wanyama;[#Law 26:25; Yer 33:12; Eze 5:12; 25:13; Hos 4:3]

18wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala mabinti; bali wao wenyewe tu wataokoka.

19Au nikituma tauni katika nchi ile, na kumwaga ghadhabu yangu juu yake, kwa damu; ili kuwakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama;[#2 Sam 24:15; Eze 7:8; Ufu 16:3-6]

20wajapokuwamo ndani yake Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawangeokoa watoto wa kiume au wa kike; watajiokoa nafsi zao tu kwa haki yao.

21Maana Bwana MUNGU asema hivi; Je! U zaidi sana nitakapoleta hukumu zangu nne zilizo kali juu ya Yerusalemu, yaani, upanga, na njaa, na wanyama wabaya, na tauni, niwakatilie mbali nayo wanadamu na wanyama?[#Yer 15:2,3; Eze 5:17; Amo 4:10; Ufu 6:8]

22Lakini, tazama, watasalia mabaki watakaochukuliwa nje, wana na mabinti; tazama, watawatokea ninyi, nanyi mtaiona njia yao na matendo yao; nanyi mtafarijika katika habari ya mabaya niliyoleta juu ya Yerusalemu, naam, katika habari ya mambo yote niliyoleta juu yake.[#Eze 6:8; 20:43]

23Nao watawafariji ninyi, mtakapoona njia yao na matendo yao; nanyi mtajua ya kuwa sikufanya bila sababu mambo yote niliyoutenda, asema Bwana MUNGU.[#Yer 22:8,9]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya