The chat will start when you send the first message.
1Neno la BWANA likanijia, kusema,
2Mwanadamu, uelekeze uso wako Yerusalemu, ukadondoze neno lako upande wa mahali patakatifu, ukatabiri juu ya nchi ya Israeli;[#Eze 20:46; Kum 32:2; Amo 7:16; 1 Pet 4:17]
3uiambie nchi ya Israeli, BWANA asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, nami nitautoa upanga wangu alani, nami nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya.[#Ayu 9:22]
4Basi, kwa kuwa nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mwovu, upanga wangu utatoka alani mwake, uwe juu ya watu wote wenye mwili toka kusini hadi kaskazini,[#Eze 20:47]
5na watu wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimeufuta upanga wangu alani mwake; hautarudi tena.[#Isa 45:23]
6Piga kite, basi, Ee mwanadamu; kwa kuvunjika moyo na uchungu mwingi mbele ya macho yao.[#Isa 22:4]
7Na itakuwa, wakuambiapo, Mbona unapiga kite? Ndipo utakaposema, Kwa sababu ya habari hizo, maana linakuja; na kila moyo utayeyuka, na mikono yote itakuwa dhaifu, na kila roho itazimia, na magoti yote yatageuka kuwa kama maji; tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU.
8Neno la BWANA likanijia, kusema,
9Mwanadamu, tabiri, useme, BWANA asema hivi; Nena, Upanga, upanga, umenolewa na kusuguliwa,[#Kum 32:41]
10umenolewa ili kufanya machinjo; umesuguliwa ili uwe kama umeme; basi je! Tufanye furaha? Upanga unadharau fimbo ya mwanangu, kama unavyodharau kila mti.
11Nao umetolewa ili ung'arishwe upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye.
12Piga kelele, utoe sauti ya uchungu, Ee mwanadamu, kwa maana upanga u juu ya watu wangu, u juu ya wakuu wote wa Israeli; wametolewa wauawe na upanga pamoja na watu wangu, basi, jipige pajani.[#Yer 31:19]
13Kwa maana kuna kujaribiwa; itakuwaje, basi, ikiwa upanga unaidharau hiyo fimbo? Haitakuwapo tena; asema Bwana MUNGU.[#Ayu 9:23]
14Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote.[#1 Fal 20:30; Eze 8:12]
15Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje.
16Jiweke tayari, nenda upande wa kulia; jipange, nenda upande wa kushoto; mahali popote utakapouelekeza uso wako.[#Eze 14:17]
17Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, BWANA, nimenena neno hili.[#Eze 22:13; 16:42; Kum 28:63; Isa 1:24]
18Neno la BWANA likanijia tena, kusema,
19Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini.
20Utachora njia, ili upanga upate kufikia Raba wa wana wa Amoni, na kufikia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma.[#Kum 3:11; 2 Sam 12:26; Yer 49:2]
21Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huku na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini.
22Katika mkono wake wa kulia alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome.[#Yer 51:14; Eze 4:2]
23Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe.[#Eze 17:13]
24Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa mmeufanya uovu wenu ukumbukwe, kwa maana makosa yenu yamefunuliwa, hata dhambi zenu zikaonekana kwa matendo yenu; kwa sababu mmekumbukwa, mtakamatwa kwa mkono.
25Na wewe, Ewe mtu mwovu, uliyetiwa jeraha kiasi cha kukuua, mkuu wa Israeli, ambaye siku yako imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho;[#Mwa 13:13]
26Bwana MUNGU asema hivi; Kiondoe kilemba, livue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka.[#Lk 1:52]
27Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa.[#Mwa 49:10]
28Nawe, mwanadamu, tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi, kuhusu wana wa Amoni, na kuhusu aibu yao; Nena, Upanga; upanga umefutwa; umeng'arishwa, ili kuua, ili kuufanya uue sana, upate kuwa kama umeme;[#Yer 49:1-6; Eze 25:1-7; Amo 1:3-15; Sef 2:8-11]
29wakati wanapokupa maono ya udanganyifu, wakati wanapokuagulia uongo, wanakuweka juu ya shingo zao wachukizao, na waovu, ambao siku yao imekuja, katika wakati wa adhabu ya mwisho.
30Uurudishe alani mwake. Mahali pale ulipoumbwa, katika nchi uliyozaliwa; nitakuhukumu wewe.
31Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu yako; nitakupulizia moto wa hasira yangu; nami nitakutia katika mikono ya watu walio kama hayawani, wajuao sana kuangamiza.
32Utakuwa kuni za kutiwa motoni; damu yako itamwagika katikati ya nchi; hutakumbukwa tena; maana mimi, BWANA, nimenena neno hili.