Ezekieli 24

Ezekieli 24

Chungu kitokotacho

1Tena, katika mwaka wa tisa, mwezi wa kumi, siku ya kumi ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema,

2Mwanadamu, liandike jina la siku hii, naam, la siku ii hii; mfalme wa Babeli ameuzingira Yerusalemu siku ii hii.[#2 Fal 25:1; Yer 52:4; 39:1]

3Ukawatungie mithali nyumba ya kuasi, ukawaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Teleka sufuria, liteleke; ukatie maji ndani yake;[#Zab 78:2; Mik 2:4; Eze 17:12; 11:3; Mk 12:12; Lk 8:10; Yer 1:13]

4vikusanye vipande vyake ndani yake, naam, kila kipande chema, paja na bega; lijaze mifupa iliyochaguliwa.

5Uwatwae wateule wa kundi la kondoo, ukafanye chungu ya mifupa chini yake; ukalitokose sana; naam, mifupa yake itokoswe ndani yake.

6Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Hilo sufuria ambalo kutu yake i ndani yake, ambalo kutu yake haikulitoka; litoe kipande kipande; hapana kura iliyoanguka juu yake.[#2 Fal 21:16; Eze 22:3; Mik 7:2; Nah 3:1; Yoe 3:3; Oba 1:11; Nah 3:10]

7Maana damu yake imo ndani yake; aliiweka juu ya jabali lililo wazi; hakuimwaga juu ya nchi, apate kuifunika kwa mavumbi;[#Law 17:13; Kum 12:16]

8ili ipandishe ghadhabu ya kulipa kisasi, nimeiweka damu yake juu ya jabali lililo wazi, isipate kufunikwa.[#Yer 16:17; Mt 7:2]

9Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Mimi nami nitaiongeza chungu.[#Nah 3:1; Hab 2:12]

10Tia kuni nyingi, uchochee moto, itokose nyama sana, fanyiza mchuzi mzito, mifupa ikateketee.

11Kisha litie juu ya makaa yake, tupu, lipate moto, na shaba yake iteketee, uchafu wake uyeyushwe, na kutu yake iteketee.[#Eze 22:15]

12Amejidhoofisha kwa taabu, lakini kutu yake nyingi haikumtoka; kutu yake haitoki kwa moto.

13Katika uchafu wako mna uasherati, kwa maana nimekusafisha, ila wewe hukusafika; hutasafishwa tena uchafu wako ukutoke, hadi nitakapokuwa nimeituliza hasira yangu kwako.[#Amo 4:6; Eze 5:13; 8:18]

14Mimi, BWANA, nimenena neno hili, nalo litakuwa; nami nitalifanya; sitaachilia, wala sitahurumia, wala sitajuta; kulingana na njia zako, na kulingana na matendo yako, ndivyo watakavyokuhukumu, asema Bwana MUNGU.[#Hes 23:19; 1 Sam 15:29; Zab 33:9; Eze 5:11]

Kufiwa kwa Ezekieli

15Neno la BWANA likanijia tena, kusema,

16Mwanadamu, tazama, ninakuondolea kwa pigo moja tunu, mteule wa macho yako; walakini hutaomboleza wala kulia, wala yasichuruzike machozi yako.

17Piga kite lakini si kwa sauti ya kusikiwa; usifanye matanga kwa ajili yake yeye aliyekufa; jipige kilemba chako, ukavae viatu vyako, wala usiifunike midomo yako, wala usile chakula cha watu.[#Hes 20:29; Yer 16:5; Law 10:6; 2 Sam 15:30; Mik 3:7]

18Basi nilisema na watu asubuhi, na jioni mke wangu akafa; nami kesho yake asubuhi nilifanya kama nilivyoagizwa.

19Watu hao wakaniambia, Je! Hutaki kutuambia maana ya mambo haya kwetu, hata umefanya kama vile ufanyavyo.[#Eze 12:9]

20Nikawaambia, Neno la BWANA lilinijia, kusema,

21Uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Angalieni, nitapatia unajisi patakatifu pangu, fahari ya uwezo wenu, mahali pa kutamaniwa na macho yenu, ambapo roho zenu zinapahurumia na wana wenu na binti zenu, mliowaacha nyuma, wataanguka kwa upanga.[#Yer 7:14; Eze 7:20; Zab 27:4]

22Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya; hamtaifunika midomo yenu, wala kula chakula cha watu.[#Yer 16:6]

23Na vilemba vyenu vitakuwa juu ya vichwa vyenu, na viatu vyenu miguuni mwenu; hamtaomboleza wala kulia; lakini mtafifia katika maovu yenu, na kusikitika kila mtu pamoja na mwenziwe.[#Ayu 27:15; Zab 78:64; Law 26:39; Eze 33:10]

24Basi ndivyo Ezekieli atakavyokuwa ishara kwenu; ninyi mtatenda sawasawa na yote aliyoyatenda yeye; litakapokuja jambo hili, ndipo mtakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.[#Isa 20:3; Yer 17:15; Eze 12:6; 25:5; Yn 13:19]

25Nawe, mwanadamu, je! Haitakuwa hivi katika siku hiyo nitakapowaondolea nguvu zao, na furaha ya utukufu wao, na kilichotamaniwa na macho yao, ambacho walikiinulia mioyo yao, watoto wao wa kiume na watoto wao wa kike,

26kwamba katika siku iyo hiyo yeye atakayeokoka atakuja kwako, akusikize jambo hili kwa masikio yako?

27Siku hiyo kinywa chako kitafumbuliwa kwake aliyeokoka, nawe utasema; hutakuwa bubu tena; ndivyo utakavyokuwa ishara kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.[#Eze 3:26]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya