The chat will start when you send the first message.
1Neno la BWANA likanijia tena, kusema,
2Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu.[#Kum 8:14; 2 Nya 26:16; Mit 16:18; Dan 5:22,23; Isa 2:12; 31:3; 1 Tim 3:6; Zab 9:20]
3Tazama, una hekima kuliko Danieli; hapana neno la siri watu wawezalo kukuficha;[#Dan 2:48; Zek 9:2]
4kwa hekima yako na kwa fahamu zako umejipatia utajiri, nawe umepata dhahabu na fedha katika hazina zako;
5kwa hekima yako nyingi, na kwa biashara yako, umeongeza utajiri wako, na moyo wako umeinuka kwa sababu ya utajiri wako;[#Kum 8:12-14]
6basi, kwa hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu;[#Dan 7:25,26; Mdo 12:22; 2 The 2:4]
7basi, tazama, nitaleta wageni juu yako, watu wa mataifa wenye kutisha; nao watafuta panga zao juu ya uzuri wa hekima yako, nao watautia uchafu mwangaza wako.[#Eze 30:11]
8Watakushusha hadi shimoni; nawe utakufa kifo chao waliouawa kati ya bahari.
9Je! Utazidi kusema mbele yake huyo akuuaye, Mimi ni mungu? Lakini u mwanadamu, wala si Mungu, mkononi mwake akutiaye jeraha.
10Utakufa kifo cha hao wasiotahiriwa, kwa mikono ya wageni; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.[#Eze 31:18]
11Tena neno la BWANA likanijia, kusema,
12Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia mhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri.[#Eze 27:3]
13Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.[#Mwa 2:8; 3:23,24; Eze 31:8,9; 26:13; Yoe 2:3]
14Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nilikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huku na huko kati ya mawe ya moto.[#Kut 25:20; Eze 20:40]
15Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako.
16Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto.
17Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.[#2 Pet 2:6; Yud 1:7]
18Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao.[#Amo 1:10]
19Wote wakujuao kati ya makabila ya watu watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele.
20Neno la BWANA likanijia, kusema,[#Yoe 3:4-8; Zek 9:1-2; Mt 11:21-22; Lk 10:13-14]
21Mwanadamu, uuelekezee Sidoni uso wako, ukatabiri juu yake,[#Isa 23:4,12; Yer 25:22; Eze 32:30]
22useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Sidoni, nami natukuzwa kati yako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimetekeleza hukumu zangu ndani yake, na kutakasika ndani yake.[#Kut 14:4; Zab 9:16; Eze 39:13; 20:41]
23Maana nitampelekea tauni, na damu, katika njia kuu zake, na hao waliotiwa jeraha wataanguka kati yake, kwa upanga juu yake pande zote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.[#Eze 38:22]
24Wala hautakuwapo mchongoma uchomao kwa nyumba ya Israeli; wala mwiba uumizao miongoni mwa wote wamzungukao, waliowatenda mambo ya jeuri; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.[#Hes 33:55; Yos 23:13]
25Bwana MUNGU asema hivi; Nitakapokuwa nimewakusanya nyumba ya Israeli, na kuwatoa katika watu ambao wametawanyika kati yao, na kutakasika kati yao machoni pa mataifa, ndipo watakapokaa katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu, Yakobo.[#Isa 11:12; Hos 1:11; Eze 20:41]
26Nao watakaa humo salama; naam, watajenga nyumba, na kupanda mashamba ya mizabibu, na kukaa salama; nitakapokuwa nimetekeleza hukumu zangu juu ya watu wote, wanaowatenda mambo ya jeuri pande zote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao.[#Isa 65:21; Amo 9:14; Yer 31:5]