Ezekieli 45

Ezekieli 45

Wilaya takatifu

1Tena, mtakapoigawanya nchi kwa kura iwe urithi, mtamtolea BWANA toleo, sehemu takatifu ya nchi, urefu wake utakuwa urefu wa mianzi elfu ishirini na tano, na upana wake elfu kumi; itakuwa takatifu ndani ya mipaka yake yote pande zote.[#Mit 3:9,10; Eze 48:8]

2Katika hiyo itakuwako sehemu kwa mahali patakatifu, urefu wake mia tano, na upana wake mia tano, mraba pande zote; na dhiraa ishirini kwa viunga vyake pande zote.[#Eze 42:20]

3Na kwa kipimo hicho utapima, urefu wa elfu ishirini na tano, na upana wa elfu kumi; na ndani yake patakuwa patakatifu, palipo patakatifu sana.

4Hiyo ni sehemu takatifu ya nchi; itakuwa ya makuhani, wahudumu wa patakatifu, wakaribiao kumhudumia BWANA; nayo itakuwa mahali kwa nyumba zao, na patakatifu kwa mahali patakatifu.[#Eze 44:15]

5Tena urefu wa elfu ishirini na tano, na upana wa elfu kumi, ni sehemu ya Walawi, wahudumu wa nyumba, iwe milki yao wenyewe kwa vyumba ishirini.[#Eze 48:13; 40:17]

6Nanyi mtaiandika milki ya mji, upana wake elfu tano, na urefu wake elfu ishirini na tano, kandokando ya mahali palipotolewa, iwe sehemu takatifu; nayo itakuwa ya nyumba yote ya Israeli.

7Na sehemu itakayokuwa ya mkuu itakuwa upande huu, na upande huu, wa toleo takatifu, na wa milki ya mji, kulikabili toleo takatifu, na kuikabili milki ya mji, upande wa magharibi kuelekea magharibi, na upande wa mashariki kuelekea mashariki; na kwa urefu wake sawasawa na sehemu mojawapo, toka mpaka wa magharibi hadi mpaka wa mashariki.[#Zab 2:8; Eze 34:24; 46:16-18; 48:21]

8Katika nchi hiyo itakuwa milki kwake katika Israeli; wala wakuu wangu hawatawaonea watu wangu tena kabisa; bali watawapa nyumba ya Israeli nchi hiyo, kwa kadiri ya makabila yao.[#Eze 22:27; 46:18; Yer 22:17]

9Bwana MUNGU asema hivi; Na iwatoshe ninyi, enyi wakuu wa Israeli; ondoeni dhuluma na unyang'anyi; fanyeni hukumu na haki; acheni kutoza kwenu kwa nguvu katika watu wangu, asema Bwana MUNGU.[#Eze 44:6; Yer 22:3]

10Mtakuwa na mizani ya haki, na efa ya haki, na bathi ya haki.[#Mit 11:1; Law 19:36]

11Efa na bathi zitakuwa za kipimo kimoja; ili kwamba bathi ichukue sehemu ya kumi ya homeri, na efa sehemu ya kumi ya homeri; kipimo chake kitakuwa kwa kadiri ya cheo cha kawaida cha homeri.

12Nayo shekeli itakuwa gera ishirini; shekeli tano zitakuwa shekeli tano, shekeli kumi zitakuwa kumi, na shekeli hamsini zitakuwa mane yenu.[#Kut 30:13; Law 27:25]

Matoleo

13Toleo mtakalotoa ni hili; sehemu ya sita ya efa katika homeri moja ya ngano, nanyi mtatoa sehemu ya sita ya efa katika homeri ya shayiri;

14na sehemu ya mafuta iliyoamriwa, katika bathi ya mafuta, itakuwa sehemu ya kumi ya bathi katika kori moja, ambayo ni bathi kumi, yaani homeri; maana bathi kumi ni homeri moja;

15na mwana-kondoo mmoja wa kundi katika mia mbili, katika malisho ya Israeli yenye maji; kwa sadaka ya unga, na kwa sadaka ya kuteketezwa, na kwa sadaka za amani, ili kuwafanyia upatanisho, asema Bwana MUNGU.[#Law 1:4; Rum 5:10; 2 Kor 5:18,19; Efe 2:16; Kol 1:21; Tit 2:14]

16Watu wote wa nchi watatoa toleo hili kwa ajili ya mkuu katika Israeli.

17Tena itakuwa kazi ya mkuu kutoa hizo sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na sadaka za vinywaji, katika sikukuu, na katika mwezi mpya, na katika sabato, katika sikukuu zote za nyumba ya Israeli zilizoamriwa; atatengeneza sadaka ya dhambi, na sadaka ya unga, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ya Israeli.[#Yn 6:51; 2 Kor 5:21; Gal 3:13; Kol 1:20; 1 Pet 2:24]

Sikukuu

18Bwana MUNGU asema hivi; Mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, utatwaa ng'ombe dume mchanga na mkamilifu; nawe utapatakasa mahali patakatifu.[#Law 16:16; Ebr 9:22; Eze 43:22,26]

19Na kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya dhambi, na kuitia juu ya miimo ya milango ya nyumba, na juu ya pembe nne za daraja ya madhabahu, na juu ya miimo ya lango la ua wa ndani.[#Eze 43:20]

20Nawe utafanya vivyo hivyo katika mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi kwa ajili ya kila mtu akosaye, na kwa ajili ya mtu aliye mjinga, ndivyo mtakavyoifanyia nyumba upatanisho.[#Zab 19:12; Law 4:27; Rum 16:18; Ebr 5:2]

21Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, mtakuwa na Pasaka, sikukuu ya siku saba; mkate usiotiwa chachu utaliwa.[#Law 23:5,6; Kut 12:1-20; Hes 9:2,3; 28:16-25; Kum 16:1]

22Na siku hiyo mkuu atatengeneza ng'ombe kuwa sadaka ya dhambi, kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu wote wa nchi.[#Mt 20:28; 1 Pet 2:24; Law 4:14]

23Tena, katika zile siku saba za sikukuu atamtengenezea BWANA sadaka ya kuteketezwa, ng'ombe saba na kondoo dume saba wakamilifu, kila siku kwa muda wa siku saba, na beberu mmoja kila siku kuwa sadaka ya dhambi.[#Law 23:8; Hes 28:15]

24Naye atatengeneza sadaka ya unga, efa moja kwa ng'ombe, na efa moja kwa kondoo dume, na hini moja ya mafuta kwa efa moja;[#Eze 46:5,7]

25katika mwezi wa saba, siku ya kumi na tano ya mwezi, katika sikukuu atafanya vivyo hivyo kwa muda wa siku saba; sadaka ya dhambi vivyo hivyo, na sadaka ya kuteketezwa vivyo hivyo, na sadaka ya unga vivyo hivyo, na mafuta vivyo hivyo.[#Kum 16:13; Law 23:33-36; Hes 29:12-38]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya