Wagalatia 6

Wagalatia 6

Chukulianeni mizigo

1Ndugu zangu, mtu akishikwa katika kosa lolote, ninyi mlio wa Roho mrejesheni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.[#Mt 18:15; Yak 5:19]

2Mchukuliane mizigo na hivyo kuitimiza sheria ya Kristo.

3Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake.

4Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake.[#2 Kor 13:5]

5Maana kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.[#Rum 14:12]

6Mwanafunzi na amshirikishe mwalimu wake katika mema yote.[#1 Kor 9:14]

7Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.

8Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.[#Rum 8:13; Yn 6:63; 3:6]

9Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.[#2 The 3:13]

10Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.[#2 Pet 1:7]

Mawaidha ya mwisho na baraka

11Tazameni niandikavyo kwa herufi kubwa niwaandikiapo kwa mkono wangu mimi mwenyewe!

12Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu.[#Gal 5:11; Flp 3:18]

13Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu.

14Lakini mimi, la hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.[#1 Kor 1:31; 2:2]

15Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutotahiriwa, ila kiumbe kipya.[#Gal 5:6; 1 Kor 7:19]

16Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu.[#Zab 125:5; 128:6; Flp 3:3]

17Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu.[#2 Kor 4:10]

18Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya