The chat will start when you send the first message.
1Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi.[#Mwa 18:2,22]
2Akasema, Bwana zangu, karibuni nawasihi mwingie nyumbani mwa mtumwa wenu, mkalale, mkanawe miguu yenu, hata asubuhi mwondoke na mapema mkaende zenu. Wakasema, Sivyo, lakini tutakaa uwanjani usiku kucha.[#Ebr 13:2; Lk 24:28]
3Akawasihi sana, nao wakaja, wakaingia nyumbani mwake. Akawafanyia karamu, akawapikia mikate isiyochachwa nao wakala.[#Mwa 18:8]
4Hata kabla hawajalala, watu wa mji, wenyeji wa Sodoma, wakaizunguka nyumba, vijana kwa wazee, watu wote waliotoka pande zote.
5Wakamwita Lutu, wakamwambia, Wako wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwalete kwetu, ili tuweze kuwajua kimwili.[#Amu 19:22-24; Isa 3:9; Mwa 4:1; Rum 1:24; Yud 1:7; #19:5 Katika Kiebrania hakuna kimwili.]
6Lutu akawatokea mlangoni, akafunga mlango nyuma yake.
7Akasema, Basi, nawasihi, ndugu zangu, msitende vibaya hivi.
8Tazama, ninao binti wawili ambao hawajajua mwanamume, nawasihi nitawatolea kwenu mkawafanyie vilivyo vyema machoni penu, ila watu hawa msiwatende neno, kwa kuwa wamekuja chini ya dari yangu.
9Wakasema, “Ondoka hapa!” Kisha wakasema, “Mtu huyu amekuja kukaa kwetu kama mgeni; naye kumbe anataka kuhukumu! Basi tutakutenda vibaya kuliko hawa”. Wakamsonga sana Lutu, wakakaribia wauvunje mlango.[#Kut 2:14; Mdo 7:26,28; 2 Pet 2:7,8]
10Lakini wale watu wakanyosha mikono yao, wakamwingiza Lutu kwao nyumbani, wakaufunga mlango.
11Kisha wakawapiga hao watu walioko mlangoni kwa upofu, wadogo kwa wakubwa, hata wakashindwa kuupata mlango.[#2 Fal 6:18; Mdo 13:11]
12Basi wale watu wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Wakwe, wanao wa kiume au wa kike, na wowote ulio nao katika mji uwatoe katika mahali hapa;[#Yos 6:22; Mwa 7:1; 2 Pet 2:9]
13maana tutapaharibu mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za BWANA; naye BWANA ametutuma tupaharibu.[#1 Nya 21:15]
14Lutu akatoka na kusema na wachumba wa binti zake, akawaambia, “Ondokeni mahali hapa kwa sababu BWANA atauharibu mji huu”. Lakini akaonekana kama achezaye machoni pa wakwe zake.[#Yer 51:6,45; Hes 16:21,45; Ufu 18:4; Kut 9:21; Lk 17:28-30; 24:11]
15Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, la sivyo utapotelea katika maangamizi ya mji huu.
16Akakawiakawia; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, kwa jinsi BWANA alivyomhurumia, wakamtoa wakamweka nje ya mji.[#2 Pet 2:7; Kut 34:7; 1 Sam 2:9; 1 Nya 16:34; Zab 25:10; 31:23; 32:10; Mit 2:8; Efe 2:4,5]
17Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde popote; ujiponye mlimani, usije ukaangamia.[#Ebr 2:3; Mwa 19:26]
18Lutu akawaambia, Sivyo, bwana wangu!
19Tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha rehema zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia mlimani nisipatwe na yale mabaya, nikafa.[#1 Tim 1:14-16]
20Basi mji huu u karibu, niukimbilie, nao ni mdogo, nijiponye sasa huko, sio mdogo huu? Na nafsi yangu itaishi.
21Akamwambia, Tazama, nimekukubali hata kwa neno hili, kwamba sitauangamiza mji huo uliounena.
22Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lolote, hadi uingiapo humo. Kwa hiyo jina la mji ule likaitwa Soari.[#Mwa 13:10; 14:2; #19:22 ‘yaani mdogo’]
23Jua lilikuwa limechomoza juu ya nchi Lutu alipoingia Soari.
24Ndipo BWANA akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto kutoka mbinguni kwa BWANA.[#Mt 10:15; 11:23-24; Lk 10:12; 17:29; 2 Pet 2:6; Yud 1:7; Kum 29:23; Zab 11:6; Isa 13:19; Yer 20:16; 50:40; Eze 16:49,50; Hos 11:8; Amo 4:11; Sef 2:9]
25Akaangusha miji hiyo na Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea katika nchi ile.[#Mwa 14:3; Zab 107:34]
26Lakini mkewe Lutu, akiwa nyuma ya mumewe, aliangalia nyuma akawa nguzo ya chumvi.[#Lk 17:32]
27Abrahamu akatoka asubuhi kwenda mahali aliposimama mbele za BWANA,[#Mwa 18:22]
28naye akatazama upande wa Sodoma na Gomora na nchi yote ya hilo Bonde, akaona, na tazama, moshi wa nchi ukapanda, kama moshi wa tanuri.[#Ufu 18:9]
29Ikawa Mungu alipoiharibu miji ya Bondeni, Mungu akamkumbuka Abrahamu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo aliyokaa Lutu.[#Mwa 8:1; 18:23]
30Lutu akapanda kutoka Soari akakaa mlimani, na binti zake wawili pamoja naye, kwa sababu aliogopa kukaa katika Soari. Akakaa katika pango, yeye na binti zake wawili.[#Mwa 19:17,19]
31Yule mkubwa akamwambia mdogo, Baba yetu ni mzee, wala hakuna mwanamume katika nchi atuingilie kama ilivyo desturi ya dunia yote.[#Mwa 16:2,4; 38:8; Kum 25:5]
32Haya, na tumnyweshe baba yetu mvinyo, tukalale naye, ili tumhifadhie baba yetu uzao.[#Lk 21:34; 1 Kor 15:33; Mk 12:19]
33Wakamnywesha baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka huyo mkubwa akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka.
34Ikawa siku ya pili, mkubwa akamwambia mdogo, Tazama, nimelala jana na baba yangu, tumnyweshe mvinyo tena usiku huu, ukaingie ukalale naye ili tupate uzao kwa baba yetu.
35Wakamnywesha tena baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka mdogo akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka.
36Basi hao binti wote wawili wa Lutu wakapata mimba kwa baba yao.
37Yule mkubwa akazaa mwana, akamwita jina lake Moabu; huyo ndiye baba wa Wamoabi, hata leo.[#Kum 2:9]
38Na yule mdogo naye akazaa mwana akamwita jina lake Benami; huyo ndiye baba wa Waamoni hata leo.[#Kum 2:19]