The chat will start when you send the first message.
1Basi umri wake Sara ulikuwa miaka mia moja na ishirini na saba, ndio umri wake Sara.
2Sara akafa katika Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Abrahamu akamlilia na kumwombolezea Sara.[#Yn 11:31,35]
3Akaondoka Abrahamu kutoka mbele ya maiti wake, akasema na wazawa wa Hethi, akinena,
4Mimi ni mgeni, ninatembea kwenu; nipeni mahali pa kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele yangu.[#Ebr 11:9,13; Mdo 7:16; Mwa 17:8; 1 Nya 29:15; Zab 39:12; 105:12; 2 Kor 5:6,7; 1 Pet 1:17; 2:11; Mwa 49:30]
5Wazawa wa Hethi wakamjibu Abrahamu, wakamwambia,
6Utusikie, Ee bwana, ndiwe mtu mkuu sana kwetu, uzike maiti wako katika kaburi lile utakalochagua katika makaburi yetu. Hapana mtu kwetu atakayekuzuilia kaburi lake, usizike maiti wako.[#Mwa 13:2; 14:14]
7Abrahamu akaondoka, akainama mbele ya watu wa nchi, mbele ya hao wazawa wa Hethi.[#Rum 13:7]
8Naye akazungumza nao, akisema, Ikiwa nia yenu nimzike maiti wangu atoke mbele yangu, mnisikie, mkaniombee kwa Efroni mwana wa Sohari,
9ili kwamba anipe pango la Makpela, iliyo katika mpaka wa shamba lake, na anipe kwa kima kilicho kamili, katikati yenu, iwe milki yangu ya kuzikia.
10Basi Efroni alikuwa akiketi kati ya wazawa wa Hethi. Efroni Mhiti akamjibu Abrahamu, na wazawa wa Hethi wanasikiliza, hata watu wote waingiao mlango wa mji wake, akisema,[#Mwa 34:20,24; Rut 4:4]
11Sivyo, bwana wangu, unisikilize. Lile shamba nakupa, na pango lililomo nakupa; mbele ya wana wa watu wangu nakupa, uzike maiti wako.[#2 Sam 24:20-24]
12Abrahamu akainama mbele ya watu wa nchi.
13Akamwambia Efroni, na watu wa nchi wanasikiliza, akisema, Tafadhali unisikilize; nitatoa kima cha shamba, nawe ukipokee kwangu, nami nitamzika humo maiti wangu.[#Flp 4:5-8]
14Efroni akamjibu Abrahamu, akamwambia,
15Bwana wangu, unisikilize. Sehemu ya nchi, ambayo thamani yake ni shekeli za fedha mia nne, ni nini hii baina yako na yangu? Basi uzike maiti wako.[#Kut 30:13; Eze 45:12]
16Abrahamu akakubali maneno ya Efroni. Abrahamu akampimia Efroni ile fedha aliyotaja masikioni mwa wazawa wa Hethi, shekeli za fedha mia nne za namna inayotumika na wenye biashara.[#Yer 32:9-12]
17Basi shamba la Efroni lililokuwa katika Makpela kuelekea Mamre, shamba, na pango lililokuwemo, na miti yote iliyokuwamo shambani, iliyokuwa katika mipaka yake pande zote, vyote viliyakinishwa[#Mwa 25:9; 49:30; Mdo 7:16]
18kuwa mali yake Abrahamu, mbele ya wazawa wa Hethi, mbele ya watu wote waingiao katika mlango wa mji wake.
19Basi baada ya hayo Abrahamu akamzika Sara mkewe katika pango la shamba la Makpela kuelekea Mamre, ndiyo Hebroni, katika nchi ya Kanaani.[#Mwa 35:29]
20Na lile shamba, na pango lililomo, iliyakinishwa kuwa mali yake Abrahamu na wazawa wa Hethi, kuwa mahali pa kuzikia.[#Rut 4:7-10; Yer 32:10,11]