Mwanzo 25

Mwanzo 25

Wazawa wa Ketura

1Abrahamu alioa mke mwingine jina lake akiitwa Ketura.

2Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na Midiani, na Ishbaki, na Sua.[#1 Nya 1:32]

3Yokshani akamzaa Sheba, na Dedani; na wana wa Dedani walikuwa Waashuri na Waletushi, na Waleumi.

4Na wana wa Midiani walikuwa, Efa, na Eferi, na Hanoki, na Abida, na Eldaa.

Hao wote walikuwa ni wana wa Ketura.

5Abrahamu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo.[#Mwa 24:36]

6Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Abrahamu, Abrahamu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu.[#Mwa 21:14; Amu 6:3]

Kifo cha Abrahamu

7Abrahamu aliishi miaka mia moja na sabini na mitano.

8Abrahamu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake.[#Mwa 15:15; 47:8,9; 35:29; 49:33; Mdo 13:36]

9Isaka na Ishmaeli wanawe wakamzika katika pango ya Makpela, katika shamba la Efroni mwana wa Sohari Mhiti, lielekealo Mamre.[#Mwa 49:29,30; 50:13]

10Katika lile shamba alilolinunua Abrahamu kwa wazawa wa Hethi, huko ndiko alikozikwa Abrahamu na Sara mkewe.[#Mwa 23:3-16]

11Ikawa, baada ya kufa kwake Abrahamu, Mungu akambariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akakaa karibu ya Beer-lahai-roi.[#Mwa 16:14; 24:62]

Uzao wa Ishmaeli

12Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli, mwana wa Abrahamu, ambaye Hajiri, Mmisri, mjakazi wa Sara, alimzalia Abrahamu.[#1 Nya 1:29]

13Na haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, kwa majina yao, na kwa vizazi vyao.

Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli, ni Nebayothi, na Kedari, na Abdeeli, na Mibsamu,

14na Mishma, na Duma, na Masa,

15na Hadadi, na Tema, na Yeturi, na Nafishi, na Kedema.

16Hao ndio wana wa Ishmaeli, na hayo ni majina yao, katika miji yao, na katika vituo vyao, maseyidi kumi na wawili kwa kufuata jamaa zao.[#Mwa 17:20]

17Ishmaeli aliishi miaka mia moja na thelathini na saba. Akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake.[#Mwa 25:8; 49:33; Mk 15:37]

18Wakakaa toka Havila mpaka Shuri, unaoelekea Misri, kwa njia ya kwenda Ashuru. Akakaa katikati ya ndugu zake wote.[#1 Sam 15:7; Mwa 16:12]

Kuzaliwa na kukua kwa Esau na Yakobo

19Na hivi ndivyo vizazi vya Isaka, mwana wa Abrahamu. Abrahamu alimzaa Isaka.[#Mt 1:2]

20Isaka akawa mwenye miaka arubaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake.[#Mwa 22:23; 24:29,67]

21Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.[#1 Sam 1:11; 1 Nya 5:20; 2 Nya 33:13; Ezr 8:23; Rum 9:10]

22Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA.[#1 Sam 9:9; 10:22]

23BWANA akamwambia,[#Rum 9:12; Mwa 24:60]

Mataifa mawili yako tumboni mwako,

Na makabila mawili ya watu watafarakana tangu tumboni mwako.

Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili,

Na mkubwa atamtumikia mdogo.

24Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake.

25Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau.[#Mwa 27:11]

26Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa.[#Hos 12:3; Mwa 27:36]

27Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani.[#Mwa 27:3,5; Ayu 1:1,8; 2:3; Ebr 11:9]

28Basi Isaka akampenda Esau, kwa sababu alikula mawindo yake, na Rebeka akampenda Yakobo.[#Mwa 27:6,19]

Esau auza haki ya uzawa wake

29Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka mbugani, naye alikuwa amechoka sana.

30Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu.[#25:30 maana yake ni Mwekundu.]

31Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza.

32Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi?

33Yakobo akamwambia, Niapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza.[#Ebr 12:16]

34Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.[#1 Kor 15:32]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya