Mwanzo 35

Mwanzo 35

Yakobo arudi Betheli

1Mungu akamwambia Yakobo, Ondoka, panda uende Betheli, ukakae huko; ukamfanyie Mungu madhabahu huko; yeye aliyekutokea ulipomkimbia Esau, ndugu yako.[#Mwa 28:11-17,19; 27:43; 28:13]

2Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu.[#Mwa 31:19; Yos 24:15; 1 Sam 7:3; Kut 19:10]

3Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea.[#Mwa 32:7,24; Zab 107:6; Mwa 28:20; 31:3,42]

4Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na vipuli vilivyokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu.[#Hos 2:13; Yos 24:26]

5Wakashika njia, hofu ya Mungu ikaishika miji iliyowazunguka, wala hawakuwafuata wana wa Yakobo.[#Kut 15:16; 23:27; Kum 11:25; Yos 2:9; 5:1; 2 Nya 14:14]

6Basi Yakobo akafika Luzu, katika nchi ya Kanaani, ndio Betheli, yeye na watu wote waliokuwa pamoja naye.[#Mwa 28:22]

7Akajenga huko madhabahu, akapaita mahali pale, El-Betheli; kwa sababu huko Mungu alimtokea, hapo alipomkimbia ndugu yake.[#Mhu 5:4; Mwa 28:13]

8Akafa Debora mlezi wa Rebeka, akazikwa chini ya Betheli, chini ya mwaloni; na jina lake likaitwa Alon-bakuthi.[#Mwa 24:59; #35:8 maana yake ni Mwaloni wa Vilio.]

9Mungu akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki.[#Hos 12:4]

10Mungu akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli.[#Mwa 17:5; 32:28]

11Mungu akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uzidi ukaongezeke. Taifa na kundi la mataifa watatoka kwako, na wafalme watatoka katika uzao wako.[#Mwa 17:4-8; 48:3,4; Kut 6:3; #35:11 Katika Kiebrania ni viunoni mwako.]

12Na nchi hii niliyowapa Abrahamu na Isaka nitakupa wewe, na uzao wako baada yako nitawapa nchi hiyo.[#Mwa 12:7; 13:15; 28:13; Kut 32:13]

13Mungu akakwea juu kutoka kwake mahali hapo aliposema naye.[#Mwa 17:22]

14Yakobo akasimamisha nguzo mahali aliposema naye, nguzo ya mawe, akamimina juu yake sadaka ya kinywaji, akamimina mafuta juu yake.[#Mwa 28:18-19]

15Yakobo akapaita mahali pale, Mungu aliposema naye, Betheli.

Kuzaliwa kwa Benyamini na kufa kwa Raheli

16Wakasafiri kutoka Betheli, na kabla ya kufika Efrata, Raheli akashikwa na uchungu wa kuzaa, na uchungu wake ulikuwa mkali.

17Ikawa alipokuwa anashikwa sana na uchungu, mkunga akamwambia, Usiogope, maana sasa utamzaa mwanamume mwingine.[#Mwa 30:24]

18Ikawa hapo katika kutoa roho yake, maana alikufa, akamwita jina lake Benoni, lakini babaye alimwita Benyamini.

19Akafa Raheli, akazikwa katika njia ya Efrata, ndio Bethlehemu.[#Mwa 48:7; Rut 1:2; 4:11; Mik 5:2; Mt 2:6]

20Yakobo akasimamisha nguzo juu ya kaburi lake, ndiyo nguzo ya kaburi la Raheli hata leo.[#1 Sam 10:2]

21Kisha akasafiri Israeli akapiga hema yake upande wa pili wa mnara wa Ederi.[#Mik 4:8]

22Ikawa Israeli alipokuwa akikaa katika nchi ile, Reubeni akaenda akalala na Bilha, suria wa babaye; Israeli akasikia habari.[#Mwa 49:4; 1 Nya 5:1]

Basi hao wana wa Yakobo walikuwa kumi na wawili.

23Wana wa Lea ni Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, na Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Zabuloni.[#Mwa 46:8; Kut 1:2]

24Wana wa Raheli, ni Yusufu na Benyamini.

25Wana wa Bilha, kijakazi wa Raheli, ni Dani na Naftali.

26Wana wa Zilpa, kijakazi wa Lea, ni Gadi na Asheri. Hawa ndio wana wa Yakobo aliozaliwa katika Padan-aramu.

Kufa kwa Isaka

27Yakobo akaja kwa Isaka, babaye, huko Mamre, mji wa Arba, ndio Hebroni, walipokaa ugenini Abrahamu na Isaka.[#Mwa 13:18; Yos 14:15]

28Siku za Isaka zilikuwa miaka mia moja na themanini.

29Naye Isaka akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake, ni mzee, ameshiba siku. Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika.[#Mhu 12:7; Mwa 15:15; 25:8,9; 49:31]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya