Mwanzo 37

Mwanzo 37

Ndoto za Yusufu

1Yakobo akakaa katika nchi aliyosafiri baba yake, katika nchi ya Kanaani.[#Mwa 36:7]

2Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya.[#1 Sam 2:22-24]

3Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu.[#2 Sam 13:18]

4Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani.[#Mwa 27:41; 49:23; 1 Sam 17:28; Yn 7:3,5; 1 Yoh 2:11; 3:10]

5Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia;

6akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota.

7Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.[#Mwa 42:6; 43:26; 44:14]

8Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake.

9Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia.[#Mwa 46:29]

10Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie mpaka chini?[#Mwa 27:29]

11Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.[#Mdo 7:9; Lk 2:19,51]

Yusufu auzwa na ndugu zake

12Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu.

13Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa.

14Akamwambia, Nenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akamtuma kutoka bonde la Hebroni, na akafika Shekemu.[#Mwa 29:6; 1 Sam 17:18; Mwa 13:18]

15Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazungukazunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini?

16Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga.[#Wim 1:7]

17Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani.[#2 Fal 6:13]

18Wakamwona akiwa mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue.[#1 Sam 19:1; Zab 31:13; Mt 27:1; Mk 14:1; Yn 11:53; Mdo 23:12]

19Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja.

20Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika shimo mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.[#Mit 1:11; 6:17; 1 Yoh 3:12,13]

21Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue.[#Mwa 42:22]

22Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika shimo hili lililopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake.

23Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa,

24wakamtwaa wakamtupa katika shimo; na hilo shimo ilikuwa tupu, hamna maji.

25Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri.[#Mit 30:20; Amo 6:6; Yer 8:22]

26Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake?[#Mwa 4:10; Ayu 16:18]

27Haya, na tumuuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali.[#1 Sam 18:17; Mwa 29:14; 42:21]

28Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika shimo, wakamuuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.[#Mdo 7:9; Mwa 39:1; Amu 6:3; Mwa 45:4,5; Zab 105:17; Mt 27:9]

29Akarudi Reubeni birikani, kumbe! Yusufu hayumo katika birika, akararua nguo zake.[#Ayu 1:20]

30Akarudi kwa ndugu zake, akasema, Mtoto hayuko, nami niende wapi?[#Yer 31:15; Mwa 42:13,36]

31Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu.

32Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo.[#Mwa 37:23]

33Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa.[#Mwa 44:28]

34Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi.[#Mwa 37:29]

35Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitashuka kaburini kwa mwanangu, nikiomboleza. Basi baba yake akamlilia.[#2 Sam 12:17; Mwa 42:38]

36Nao Wamidiani wakamuuza huko Misri, kwa Potifa, mmoja wa maofisa wa Farao, mkuu wa askari walinzi.[#Mwa 39:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya