Mwanzo 39

Mwanzo 39

Yusufu na mke wa Potifa

1Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri, naye Potifa, ofisa wa Farao, mkuu wa askari walinzi, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko.[#Mwa 37:28,36; Zab 105:17]

2BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri.[#Mdo 7:9; Mwa 21:22; 28:15; 1 Sam 16:18; 18:14; Zab 5:12; Mit 3:7-10; 30:5]

3Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake.[#Zab 1:3; Mit 10:6,22; 28:20]

4Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake.[#Mwa 18:3; 19:19; 24:2]

5Ikawa tokea wakati alipomweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Baraka za BWANA zikawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.[#Mwa 30:27]

6Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu chochote chake, ila hicho chakula alichokula tu.[#1 Sam 16:12]

Naye Yusufu alikuwa mtu mzuri, na mwenye uso mzuri.

7Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami.[#2 Sam 13:11]

8Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu.

9Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu chochote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nimkosee Mungu?[#Mit 6:29; Mwa 20:6; Law 6:2; 2 Sam 12:13; Zab 51:4]

10Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala kuwa naye.

11Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani afanye kazi yake, na hapakuwa na mtu yeyote kati ya wale wa nyumbani karibu;

12huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje.[#Mit 7:13]

13Ikawa alipoona ya kwamba amemwachilia nguo yake mkononi mwake, naye amekimbia nje,

14akawaita watu wa nyumbani mwake, akasema nao, akinena, Angalieni, ametuletea mtu Mwebrania atufanyie dhihaka. Ameingia kwangu ili alale nami, nikalia kwa sauti kuu.

15Ikawa, aliposikia ya kuwa nimepaza sauti yangu na kulia, aliiacha nguo yake kwangu, akakimbia, akatoka nje.

16Basi akaiweka ile nguo kwake hata bwana wake aje nyumbani.

17Naye akamwambia maneno yayo hayo, akisema, Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia kwangu anidhihaki.[#Kut 23:1; Zab 120:3; Mit 6:25; 23:27; 26:28]

18Ikawa nilipopaza sauti yangu, nikalia, akaacha nguo yake kwangu akakimbia nje.

19Ikawa bwana wake aliposikia maneno aliyoambia na mkewe, akisema, Mtumwa wako amenitendea mambo kama haya, hasira yake ikawaka.[#Mit 6:34]

20Bwana wake akamtwaa Yusufu, akamtia gerezani, mahali wafungwa wa mfalme walimokuwa wamefungiwa, naye akawa humo gerezani.[#Mwa 40:3; 41:14; Zab 105:18; 1 Pet 2:19]

21Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza.[#Mdo 7:9; Kut 3:21; 11:3; 12:36; Zab 106:46; Mit 16:7; Dan 1:9]

22Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliokuwemo gerezani; na yote yaliyofanywa humo, yeye ndiye aliyeyafanya.[#Mwa 40:3,4]

23Wala mkuu wa gereza hakufuatilia kazi liliyokuwa mikononi mwa Yusufu; kwa kuwa BWANA alikuwa pamoja naye. BWANA akayafanikisha yote aliyoyafanya.[#Mwa 39:2,3; Mit 11:11]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya