The chat will start when you send the first message.
1Basi Yakobo akaona ya kuwa kuna nafaka katika Misri, Yakobo akawaambia wanawe, Kwa nini mnatazamana?[#Mdo 7:12]
2Akasema, Angalia, nimesikia ya kuwa kuna nafaka Misri; shukeni huko mkatununulie chakula, tupate kuishi wala tusife.[#Mwa 43:8; Zab 33:18,19; Isa 38:1]
3Basi ndugu kumi wa Yusufu wakashuka Misri ili wanunue nafaka.
4Lakini Benyamini, ndugu wa Yusufu, Yakobo hakumpeleka pamoja na ndugu zake, maana alisema, Mabaya yasimpate.[#Mwa 42:38]
5Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani.[#Mwa 12:10; 26:1; Mdo 7:11]
6Naye Yusufu alikuwa ni mkuu juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake.[#Mwa 41:41; 27:29; 33:6; 37:7; Rut 2:10; 1 Fal 1:16; Isa 60:14]
7Yusufu akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema. Tumetoka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula.
8Yusufu akawatambua nduguze, bali wao hawakumtambua yeye.
9Yusufu akazikumbuka zile ndoto alizowaotea. Akawaambia, Wapelelezi ninyi, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi.[#Mwa 37:5-10]
10Wakamwambia, Hasha, bwana, watumwa wako tumekuja ili tununue chakula.
11Sisi sote ni wana wa mtu mmoja tu watu wa kweli sisi; watumwa wako si wapelelezi.
12Akawaambia, Sivyo, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi.
13Wakamwambia, Sisi watumwa wako tu ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja katika nchi ya Kanaani; na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo, na mmoja hayuko.[#Mwa 37:30; 44:20; Omb 5:7]
14Yusufu akawaambia, Ndivyo nilivyowaambia, nikisema, Wapelelezi ninyi.
15Mtabainika kwa njia hii; aishivyo Farao, hamtoki hapa, asipokuja huku huyo ndugu yenu mdogo.[#1 Sam 1:26; 17:55]
16Mtumeni mmoja wenu, aende akamlete ndugu yenu, na ninyi mtafungwa jela, hadi maneno yenu yahakikishwe kama mna kweli ninyi; ikiwa sivyo, aishivyo Farao hakika ninyi ni wapelelezi.
17Akawatia wote gerezani siku tatu.
18Siku ya tatu, Yusufu akawaambia, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu.[#Law 25:43; Neh 5:15]
19Kama ninyi ni wa kweli, mmoja wenu na afungwe gerezani, nanyi mwende mkachukue nafaka kwa ajili ya njaa ya nyumba zenu,
20mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya.[#Mwa 43:5; 44:23]
21Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosea ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia, kwa hiyo shida hii imetupata.[#Ayu 36:8,9; Hos 5:15; Zab 107:17; Mit 5:22; 11:21; Mt 7:2]
22Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, Msimkosee kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo tunadaiwa damu yake.[#Mwa 9:5; 37:21-22; 1 Fal 2:32; 2 Nya 24:22; Zab 9:12; Lk 11:50,51]
23Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alizungumza nao kupitia kwa mkalimani.
24Akaenda kando, akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao.
25Yusufu akaamuru kuvijaza vyombo vyao nafaka, na kumrudishia kila mtu fedha yake katika gunia lake, na kuwapa chakula cha njiani. Na hivyo ndivyo walivyofanyiwa.[#Mt 5:44; Rum 12:17-21; 1 Pet 3:9]
26Wakawatwika punda wao nafaka yao, wakatoka huko.
27Mmoja wao alipofungua gunia lake ili ampe punda wake chakula katika nyumba ya wageni, aliiona fedha yake; kumbe! Iko kinywani mwa gunia lake.[#Mwa 43:21]
28Akawaambia nduguze, Fedha yangu imerudishwa, angalia, imo humo guniani mwangu. Mioyo yao ikazimia, wakageukiana wakitetemeka, wakasema, Ni nini hii Mungu aliyotutendea?
29Wakaja kwa Yakobo, baba yao, katika nchi ya Kanaani, wakampasha habari za yote yaliyowapata, wakisema,
30Mtu yule aliye bwana wa nchi alisema nasi kwa maneno makali, akatufanya tu wapelelezi wa nchi.[#Mwa 42:7]
31Tukamwambia, Tu watu wa kweli sisi, wala si wapelelezi.
32Sisi tu ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu. Mmoja hayuko, na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo katika nchi ya Kanaani.
33Yule mtu, bwana wa nchi, akatuambia, Kwa njia hii nitawajua kama ninyi ni watu wa kweli; ndugu yenu mmoja mwacheni huku kwangu, kachukueni nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mwende zenu.[#Mwa 42:15,19,20]
34Mkaniletee ndugu yenu mdogo; ndipo nitakapojua kama ninyi si wapelelezi, bali ni watu wa kweli; basi nitawarudishia ndugu yenu, nanyi mtafanya biashara katika nchi hii.[#Mwa 34:10]
35Ikawa walipomimina magunia yao, kumbe! Bahasha ya fedha ya kila mtu imo katika gunia lake. Nao walipoziona bahasha za fedha zao, wao na baba yao waliogopa.[#Mwa 43:21]
36Yakobo baba yao akawaambia, Mmeniondolea watoto wangu; Yusufu hayuko, wala Simeoni hayuko, na Benyamini mnataka kumchukua naye; mambo hayo yote yamenipata mimi.[#Mwa 43:14]
37Reubeni akamwambia baba yake, akasema, Uwaue wanangu wawili nisipomrudisha kwako; mtie katika mikono yangu, nami nitamrudisha kwako.
38Akasema, Mwanangu hatashuka pamoja nanyi, maana nduguye amekufa, naye amesalia peke yake; mabaya yakimpata katika njia mtakayoiendea ndipo mtakaposhusha mvi zangu kwa sikitiko mpaka kaburini.[#Mwa 37:33; 44:28-31]