Mwanzo 46

Mwanzo 46

Yakobo ahamia Misri na jamaa yake yote

1Israeli Akasafiri, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye.[#Mwa 21:31; 26:24; 28:13; 31:42]

2Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa.[#Mwa 15:1; Ayu 33:14,15]

3Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko.[#Mwa 12:2; 28:13; Kum 26:5; Kut 1:9]

4Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako.[#Mwa 28:15; 48:21; 15:16; 50:13; Kut 3:8]

5Yakobo akaondoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyotuma Farao ili kumchukua.[#Mwa 15:13; Mdo 7:15]

6Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamepata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye.[#Kum 26:5; Yos 24:4; Zab 105:23; Isa 52:4]

7Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri.

8Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli walioingia Misri, Yakobo na wanawe: Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.[#Kut 1:1; 6:14; Hes 26:5; 1 Nya 5:1]

9Na wana wa Reubeni; Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi.

10Na wana wa Simeoni; Yemueli na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli, mwana wa mwanamke Mkanaani.[#Kut 6:15; 1 Nya 4:24]

11Na wana wa Lawi; Gershoni, na Kohathi, na Merari.

12Na wana wa Yuda; Eri, na Onani, na Shela, na Peresi, na Zera; lakini Eri na Onani walikufa katika nchi ya Kanaani. Na wana wa Peresi, ni Hesroni, na Hamuli.[#Mwa 38:3,29; 1 Nya 2:5]

13Na wana wa Isakari; Tola, na Puva, na Yashubu, na Shimroni.

14Na wana wa Zabuloni; Seredi, na Eloni, na Yaleeli.

15Hao ndio wana wa Lea, aliomzalia Yakobo katika Padan-aramu, na Dina, binti yake. Wanawe wote wa kiume na kike walikuwa watu thelathini na watatu.

16Na wana wa Gadi; Sefoni, na Hagi, na Shuni, na Esboni, na Eri, na Arodi, na Areli.[#Hes 26:15]

17Na wana wa Asheri; Imna, na Ishva, na Ishvi, na Beria, na Sera, dada yao. Na wana wa Beria ni Heberi, na Malkieli.[#1 Nya 7:30]

18Hao ndio wana wa Zilpa, ambaye Labani alimpa Lea, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao, watu kumi na sita.[#Mwa 30:10]

19Wana wa Raheli, mkewe Yakobo, Yusufu na Benyamini.

20Walizaliwa kwake Yusufu katika nchi ya Misri, Manase na Efraimu, aliomzalia Asenathi binti Potifera, kuhani wa Oni.[#Mwa 41:50-52]

21Na wana wa Benyamini; Bela, na Bekeri, na Ashbeli, na Gera, na Naamani, na Ehi, na Roshi, na Mupimu, na Hupimu, na Ardi.[#1 Nya 7:6,12]

22Hao ndio wana wa Raheli, aliomzalia Yakobo, wote walikuwa watu kumi na wanne.

23Na wana wa Dani; Hushimu.[#1 Nya 7:12]

24Na wana wa Naftali; Yaseeli, na Guni, na Yaseri, na Shilemu.[#1 Nya 7:13]

25Hao ndio wana wa Bilha, ambaye Labani alimpa Raheli, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao; wote walikuwa watu saba.[#Mwa 29:29; 30:5,7]

26Watu wote waliokuja pamoja na Yakobo mpaka Misri, waliokuwa wazawa wake, bila wake za wanawe, walikuwa watu sitini na sita.[#Kut 1:5]

27Na wana wa Yusufu aliozaliwa katika Misri walikuwa wawili. Watu wote wa nyumba ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini.[#Mdo 7:14; Kum 10:22]

Yakobo apata makao Gosheni

28Yakobo akamtuma Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni.[#Mwa 31:21]

29Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake kitambo kirefu.

30Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai.[#Lk 2:29]

31Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, Nitapanda mimi nimpashe Farao habari; nitamwambia, Ndugu zangu, na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia.

32Na watu hao ni wachungaji, maana wamekuwa watu wa kuchunga wanyama, nao wameleta kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo.

33Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu ni nini?[#Mwa 47:2,3]

34Semeni, Watumishi wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri.[#Mwa 30:35; 34:5; 37:12; Kut 8:26]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya