Mwanzo 47

Mwanzo 47

1Ndipo Yusufu akaja akamwarifu Farao, akasema, Baba yangu, na ndugu zangu, na kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo, wamekuja kutoka nchi ya Kanaani, nao wako katika nchi ya Gosheni.[#Mwa 45:10; 46:28,31]

2Akatwaa watu watano miongoni mwa nduguze, akawasimamisha mbele ya Farao.[#Mdo 7:13]

3Farao akawauliza hao nduguze, Kazi yenu ni nini? Wakamwambia Farao, Watumwa wako tu wachunga wanyama, sisi, na baba zetu.[#Mwa 46:33,34]

4Wakamwambia Farao, Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwa sababu wanyama wa watumwa wako hawana malisho, maana njaa ni nzito sana katika nchi ya Kanaani. Basi, twakusihi, uturuhusu sisi watumwa wako tukae katika nchi ya Gosheni.[#Mwa 15:13; Kum 26:5; Zab 105:23; Isa 52:4; Mwa 43:1; 46:34; Mdo 7:11]

5Farao akamwambia Yusufu, akisema, Baba yako na ndugu zako wamekujia;

6nchi ya Misri iko mbele yako, palipo pema pa nchi uwakalishe baba yako na ndugu zako; na wakae katika nchi ya Gosheni. Tena ukijua ya kuwa wako watu hodari miongoni mwao, uwaweke wawe wakuu wa wanyama wangu.

7Yusufu akamleta Yakobo babaye ndani akamweka mbele ya Farao, Yakobo akambariki Farao.[#Mwa 20:15; 1 Fal 11:28; Mit 12:24; 22:29]

8Farao akamwuliza Yakobo, Je! Siku za kuishi kwako ni ngapi?

9Yakobo akamjibu Farao, Siku za kuishi kwangu ni miaka mia moja na thelathini; siku za maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikia siku za maisha ya baba zangu katika siku za kuishi kwao.[#Zab 39:12; 119:19; 2 Kor 5:6,7; Ebr 11:9,13; 1 Pet 2:11; 1:24; Ayu 7:7; 14:1; Mhu 2:23; Yak 4:14; Mwa 25:7; 35:28]

10Yakobo akambariki Farao, akatoka mbele ya Farao.[#Mwa 47:7]

11Yusufu akawakalisha babaye na nduguze, na kuwapa milki katika nchi ya Misri, katika mahali pazuri pa nchi, katika nchi ya Ramesesi, kama Farao alivyoamuru.[#Kut 1:11; 12:37]

12Naye Yusufu akawalisha babaye na nduguze na nyumba yote ya babaye, kwa kadiri ya hesabu ya watoto wao.[#Mit 10:1; Kut 20:12]

Njaa yaikumba Misri

13Baadaye hapakuwa na chakula katika nchi yote, kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana, hata nchi ya Misri na nchi ya Kanaani zikataabika, kwa sababu ya njaa.[#Mwa 41:30; Mdo 7:11]

14Yusufu akakusanya fedha zote zilizoonekana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, kwa nafaka waliyoinunua. Yusufu akazileta zile fedha nyumbani mwa Farao.[#Mwa 41:56]

15Fedha zote zilipokwisha katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, Wamisri wote walimjia Yusufu, wakisema, Tupe sisi chakula, kwa nini tufe mbele ya macho yako? Maana fedha zetu zimekwisha.[#Mwa 47:19]

16Yusufu akasema, Toeni wanyama wenu, nami nitawapa chakula badala ya wanyama wenu, kama fedha zenu zimekwisha.

17Wakaleta wanyama wao kwa Yusufu; Yusufu akawapa chakula kwa kubadilisha na farasi, kondoo, ng'ombe na punda, naye akawalisha chakula badala ya wanyama wao wote mwaka ule.

18Na mwaka ule ulipokwisha wakamjia mwaka wa pili, wakamwambia, Hatumfichi bwana wetu ya kwamba fedha zetu zimekwisha, na makundi ya wanyama ni mali ya bwana wetu, hakikusalia kitu mbele za bwana wetu, ila miili yetu na nchi zetu.

19Kwa nini tufe mbele ya macho yako, sisi na nchi yetu? Utununue sisi na nchi yetu kwa chakula, na sisi na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao; kisha utupe mbegu, tuishi wala tusife, wala nchi yetu isipotee.

20Basi Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri; maana Wamisri waliuza kila mtu shamba lake; kwa sababu njaa ilikuwa imewazidi sana, nchi ikawa mali yake Farao.

21Akawahamisha hao watu, akawaweka katika miji, tangu upande huu wa Misri hata upande huu.

22Ila nchi ya makuhani hakuinunua; maana makuhani walikuwa na posho yao kutoka kwa Farao, wakala posho yao waliyopewa na Farao. Kwa hiyo hawakuuza nchi yao.[#Ezr 7:24]

23Yusufu akawaambia watu, Angalieni, nimewanunua leo, ninyi, na nchi yenu, kuwa mali ya Farao; basi mbegu zenu ni hizi, zipandeni katika nchi.

24Wakati wa mavuno mtampa Farao sehemu ya tano, na sehemu nne zitakaposalia zitakuwa zenu wenyewe, kuwa mbegu za nchi, na chakula chenu, na chakula chao waliomo nyumbani mwenu, na chakula cha watoto wenu.

25Wakasema, Umeyaokoa maisha yetu, na tuone kibali machoni pa bwana wetu, nasi tutakuwa watumwa wa Farao.[#Mwa 33:15]

26Yusufu akaifanya kuwa sheria ya nchi ya Misri hata leo, ya kwamba sehemu ya tano iwe mali ya Farao. Ila nchi ya makuhani tu haikuwa mali ya Farao.[#Mwa 47:22]

Siku za mwisho za Israeli

27Israeli akakaa katika nchi ya Misri, katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali humo, wakaongezeka na kuzidi sana.[#Mwa 12:2; 26:4; 46:3; Kut 1:7; Kum 26:5; Zab 105:24; Mdo 7:17]

28Yakobo akaishi katika nchi ya Misri miaka kumi na saba, basi umri wake Yakobo ulikuwa miaka mia moja na arubaini na saba.

29Siku za kufa kwake Israeli zikakaribia; akamwita mwanawe Yusufu, akamwambia, Kama nimeona kibali machoni pako, weka mkono wako chini ya paja langu, ukanifanyie rehema na kweli; nakusihi usinizike katika Misri.[#Kum 31:14; 1 Fal 2:1; Mwa 24:2,49; 50:25]

30Lakini nitakapolala pamoja na baba zangu, unichukue toka Misri, unizike katika kaburi lao. Akasema, Nitafanya kama ulivyosema.[#2 Sam 19:37; Mwa 23:2; 50:5,13; Mdo 7:16; Ebr 11:23]

31Akanena, Niapie. Naye akamwapia. Israeli akajiinamisha kwenye mchago wa kitanda.[#Mwa 48:2; 1 Fal 1:47; Ebr 11:21]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya