The chat will start when you send the first message.
1Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku zijazo.[#Kum 4:30; 33:1; Amo 3:7; Hes 24:14]
2Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo,[#Zab 34:11]
Msikilizeni Israeli, baba yenu.
3Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza,[#Kum 21:17]
Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu.
Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu.
4Umekuwa kama maji yavukavyo mpaka, basi nawe hutafana tena,[#Kum 27:20; 1 Nya 5:1]
Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako,
Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.
5Simeoni na Lawi ni ndugu;[#Mit 18:9; Mwa 34:25]
Panga zao ni silaha za jeuri.
6Nafsi yangu, usiingie katika siri yao,[#Mit 1:15; Zab 26:9]
Fahari yangu usiungane na kusanyiko lao,
Maana katika ghadhabu yao walimwua mtu,
Na kwa ukaidi wao walikata mshipa wa ng'ombe;
7Ghadhabu yao na ilaaniwe, maana ilikuwa kali,[#Yos 21:1; 1 Nya 4:24]
Na hasira yao, maana ilikuwa haina huruma.
Nitawagawa katika Yakobo,
Nitawatawanya katika Israeli.
8Yuda, ndugu zako watakusifu,
Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako.
Wana wa baba yako watakuinamia.
9Yuda ni mwanasimba,[#Hes 24:9]
Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda;
Aliinama akajilaza kama simba,
Na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha?
10Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda,[#Hes 24:17; Zab 60:7; 1 Nya 5:2; Isa 11:1; Eze 21:27; Dan 9:25; Mt 21:9; Lk 1:32; Isa 2:2; 11:10; 60:1-5; Hag 2:7; Lk 2:30; 2 Fal 18:32]
Wala mfanya sheria kati ya miguu yake,
Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki,
Ambaye mataifa watamtii.
11Atafunga punda wake katika mzabibu,
Na mwanapunda wake katika mzabibu mzuri.
Amefua nguo zake kwa mvinyo,
Na mavazi yake kwa damu ya zabibu.
12Macho yake yatakuwa mekundu kwa mvinyo,
Na meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa.
13Zabuloni atakaa pwani ya bahari,[#Kum 33:18]
Naye atakuwa kama pwani za kuegesha merikebu,
Na mpaka wake utakuwa kando ya Sidoni.
14Isakari ni punda hodari,
Ajilazaye kati ya mazizi ya kondoo;
15Akaona mahali pa raha, kuwa pema,
Na nchi, ya kuwa ni nzuri,
Akainama bega lake lichukue mizigo,
Akawa mtumishi kwa kazi ngumu.
16Dani atahukumu watu wake,[#Amu 13:2; 15:20]
Kama moja ya makabila ya Israeli;
17Dani atakuwa nyoka barabarani,[#Amu 18:27]
Bafe katika njia,
Aumaye visigino vya farasi,
Na apandaye akaanguka chali.
18Wokovu wako nimeungoja, Ee BWANA.[#Zab 25:3,5; 62:5; Isa 25:9; 40:31; Rum 2:7; 1 Kor 1:7; Flp 3:20; Tit 2:13]
19Gadi, jeshi litamsonga,[#Kum 33:20]
Lakini atawasonga wao mpaka visigino.
20Asheri, chakula chake kitakuwa kinono,
Naye atatoa tunu za kifalme.
21Naftali ni ayala aliyefunguliwa;
Anatoa maneno mazuri.
22Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa,
Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi,
Matawi yake yametanda ukutani.
23Wapiga mishale walimtenda machungu,[#Mwa 37:24]
Wakamlenga na kumbana sana
24Lakini upinde wake ukakaa imara,[#Ayu 29:20; Zab 132:2,5; 80:1; Isa 28:16]
Mikono yake ikapata nguvu,
Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo;
Kwa jina la mchungaji, yeye mwamba wa Israeli,
25Naam, kwa Mungu wa baba yako atakayekusaidia;[#Kum 33:13]
Kwa baraka za juu mbinguni.
Baraka za vilindi vilivyo chini,
Baraka za maziwa, na za mimba.
26Baraka za baba yako
Ni nyingi kuliko za milima ya kale,
Vitu vinavyotamanika vya vilima vya milele;
Na vikae juu ya kichwa cha Yusufu,
Juu ya utosi wa kichwa chake, yeye aliyeteuliwa kati ya ndugu zake.
27Benyamini ni mbwamwitu mwenye kuraruararua[#Amu 20:21,25; Hes 23:24; Est 8:11; Eze 39:10; Zek 14:1,7]
Asubuhi atakula mawindo,
Na jioni atagawanya mateka.
28Hayo yote ndiyo makabila ya Israeli kumi na mawili. Na hayo ndiyo aliyowaambia baba yao, na kuwabariki; mmoja mmoja kwa baraka zake aliwabariki.
29Akawaamuru, akasema, Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti;[#Mwa 15:15; 25:8; 2 Sam 19:37; Mwa 47:30; 50:13]
30katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Abrahamu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia.[#Mwa 23:16]
31Humo walimzika Abrahamu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami humo nikamzika Lea;[#Mwa 23:19; 25:9; 35:29]
32shamba na pango lililomo lililonunuliwa kwa wazawa wa Hethi.
33Basi Yakobo alipokwisha kuwaagiza wanawe, akakunja miguu yake kitandani, akafa, akakusanywa pamoja na watu wake.