Hosea 14

Hosea 14

Mwito wa kutubu

1Ee Israeli, mrudie BWANA, Mungu wako; maana umeanguka kwa sababu ya uovu wako.[#1 Sam 7:3,4; Hos 12:6; Isa 55:6,7]

2Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie BWANA; mkamwambie, Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo mtakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng'ombe.[#Yoe 2:17; Rum 8:26; Ebr 13:15]

3Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, Ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema.

Tumaini la kusamehewa

4Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha.

5Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni.

6Matawi yake yatatanda, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni.

7Na wao wakaao chini ya uvuli wake watarejea; watafufuka kama ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai ya Lebanoni.

8Efraimu atasema, Mimi nina nini tena na sanamu? Mimi nimeitika, nami nitamwangalia. Mimi ni kama mberoshi wenye majani mabichi. Kwangu mimi yamepatikana matunda yako.[#Yer 31:18; Yak 1:17]

9Ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za BWANA zimenyoka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake.[#Yn 18:37; Mt 11:19]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya