Hosea 8

Hosea 8

Uasi wa Israeli

1Tia baragumu kinywani mwako. Kama tai, anakuja juu ya nyumba ya BWANA; kwa sababu wamelivunja agano langu, wameiasi sheria yangu.[#Yer 4:13; Hab 1:8]

2Watanililia, Mungu wangu, sisi Israeli tunakujua.[#Zab 78:34; Mt 7:21]

3Israeli ameyatupa yaliyo mema; adui watamfuatia.

4Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nilikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali.[#1 Fal 12:16-20; 2 Fal 15:13,17,25]

5Ndama wako amemtupa, Ee Samaria; ghadhabu yangu imewaka juu yao; Wataendelea kuwa na hatia hadi lini?[#Yer 13:27]

6Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjika vipande vipande.

7Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza.

8Israeli amemezwa; sasa wamo miongoni mwa mataifa kama chombo kisichopendeza.

9Kwa maana wamekwea kwenda Ashuru, mfano wa punda wa porini aliye peke yake; Efraimu ameajiri wapenzi.[#2 Fal 15:19]

10Naam, ijapokuwa waajiri kati ya mataifa, sasa nitawakusanya; nao wanaanza kupunguka kwa sababu ya mzigo wa mfalme wa wakuu.[#Isa 10:8; Eze 26:7; Dan 2:37]

11Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake.

12Nijapomwandikia sheria yangu katika amri makumi elfu, zimehesabiwa kuwa ni kitu kigeni.[#Kum 4:6; Neh 9:13,14; Mit 22:20; Rum 3:1,2; Ayu 21:14]

13Kwa habari za dhabihu za matoleo yangu, hutoa dhabihu ya nyama na kuila; lakini BWANA hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao; watarudi kwenda Misri.

14Maana Israeli amemsahau Muumba wake, naye amejenga nyumba za enzi; na Yuda ameongeza miji yenye maboma; lakini nitatuma moto juu ya miji yake, nao utaziteketeza ngome zake.[#1 Fal 12:31]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya