Isaya 17

Isaya 17

Utabiri juu ya Dameski

1Ufunuo juu ya Dameski. Tazama, Dameski umeondolewa usiwe mji, nao utakuwa rundo la magofu.[#2 Fal 16:9; Yer 49:23-27; Amo 1:3-5; Zek 9:1]

2Miji ya Aroeri imeachwa; itakuwa mahali pa makundi ya kondoo, nao watajilaza huko wala hapana atakayewatia hofu.[#Yer 7:33]

3Na ngome ya Efraimu itakomeshwa, na ufalme wa Dameski, na mabaki ya Shamu; watakuwa kama utukufu wa wana wa Israeli, asema BWANA wa majeshi.[#Isa 7:16]

4Tena itakuwa katika siku hiyo, utukufu wa Yakobo utapungua na kunona kwa mwili wake kutakwisha.[#Isa 10:16]

5Tena itakuwa kama hapo mvunaji ashikapo mabua ya ngano, na mkono wake ukatapo masuke; tena itakuwa kama hapo mtu aokotapo masuke katika bonde la Warefai.[#Yer 51:33; Ufu 14:15-19]

6Lakini kilichosazwa na mvunaji kitakuwa ndani yake, kama vile wakati wa kupiga mizeituni, matunda mawili matatu yaliyo juu sana; matunda manne matano katika matawi, matawi ya mti wa matunda, asema BWANA, Mungu wa Israeli.

7Katika siku hiyo mwanadamu atamwangalia Muumba wake, na macho yake yatamtazama Mtakatifu wa Israeli.[#2 Nya 30:11; Zab 34:5; Hos 5:15; Mik 7:7; Zek 12:10]

8Wala hataziangalia madhabahu, kazi ya mikono yake; wala hatavitazama vilivyofanyika kwa vidole vyake, maashera na sanamu za jua.

9Katika siku hiyo miji yake yenye maboma itakuwa kama mahali palipoachwa ndani ya mwitu, na juu ya kilele cha mlima, palipoachwa mbele ya wana wa Israeli; napo patakuwa ganjo.

10Maana umemsahau Mungu wa wokovu wako, wala hukuukumbuka mwamba wa ngome yako; kwa sababu hiyo ulipanda mashamba yapendezayo, na kutia ndani yake mizabibu migeni.[#Zab 106:13,21]

11Katika siku ile ulipopanda, ulifanya kitalu, na wakati wa asubuhi ulizimeesha mbegu zako, lakini mavuno yatatoweka siku ya huzuni, na ya sikitiko la moyo lifishalo.

12Aha! Uvumi wa watu wengi!

Wanavuma kama uvumi wa bahari;

Aha! Ngurumo ya mataifa!

Wananguruma kama ngurumo ya maji mengi;

13Mataifa wananguruma kama ngurumo ya maji mengi;

Lakini atawakemea, nao watakimbia mbali sana,

Watafukuzwa kama makapi milimani mbele ya upepo,

Na kama mavumbi vuruvuru mbele ya tufani.

14Wakati wa jioni, tazama, kuna hofu;[#Amu 5:31; Mit 22:23; Zab 8:3,9]

Na kabla ya mapambazuko hawako;

Hilo ndilo fungu lao watutekao,

Na ajali yao wanaotunyang'anya mali zetu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya