Isaya 19

Isaya 19

Utabiri juu ya Misri

1Ufunuo juu ya Misri. Tazama, BWANA amepanda juu ya wingu jepesi, anafika Misri; na sanamu za Misri zinatikisika mbele zake, na moyo wa Misri unayeyuka ndani yake.[#Yer 46:2-26; Eze 29:1—32:32]

2Nami nitawaamsha Wamisri juu ya Wamisri; nao watapigana, kila mtu na ndugu yake, na kila mtu na jirani yake, mji juu ya mji, na ufalme juu ya ufalme.[#Amu 7:22; 1 Sam 14:16; 2 Nya 20:23]

3Na roho yao Misri itaondolewa, nami nitaiharibu mipango yao, nao watakwenda kwa sanamu zao, na kwa waganga, na kwa wapiga ramli na kwa wachawi.

4Nami nitawatoa hao Wamisri na kuwatia katika mikono ya bwana mgumu; na mfalme mkali atawatawala; asema Bwana, BWANA wa majeshi.

5Na maji ya baharini yatapunguka, na huo mto utakauka na kuwa pakavu.[#Yer 51:36; Eze 30:12]

6Na vijito vya mto vitatoa uvundo, na mifereji ya Misri itakuwa haina maji mengi, itakauka; manyasi na mianzi itanyauka.[#2 Fal 19:24]

7Vitu vimeavyo karibu na Nile, katika ukingo wa Nile, na vyote vilivyopandwa karibu na Nile vitakauka na kuondolewa na kutoweka.

8Na wavuvi wataugua, na wote wavuao kwa ndoana watahuzunika, nao watandao jarife juu ya maji watazimia.

9Tena wao wafanyao kazi ya kuchana kitani watafadhaika, na hao pia wafumao bafta.

10Na nguzo za nchi zitavunjika vipande vipande, wote wafanyao kazi ya mshahara watahuzunika nafsini mwao.

11Wakuu wa Soani wamekuwa wapumbavu kabisa; washauri wenye hekima wa Farao, ushauri wao umepumbazika; mwawezaje kumwambia Farao, Mimi ni mwana wa wenye hekima, ni mwana wa wafalme wa zamani?

12Wako wapi, basi, watu wako wenye hekima? Na wakuambie sasa; na wajue mambo aliyokusudia BWANA wa majeshi juu ya Misri.[#Isa 41:22,23; Mdo 7:22; 1 Kor 1:20]

13Wakuu wa Soani wamekuwa wapumbavu, wakuu wa Nofu wamedanganyika; na hao walio mawe ya pembeni ya kabila zake wameipotosha Misri.[#Yer 2:16; Hos 9:6]

14Yeye BWANA ametia roho ya ushupavu katika moyo wa Misri, nao wameikosesha Misri katika matendo yake yote, kama mlevi aendavyo huku na huko akitapika.

15Wala haitakuwako kazi yoyote katika Misri iwezayo kufanywa, ya kichwa au ya mkia, ya tawi au ya nyasi.

16Katika siku hiyo Misri itakuwa kama wanawake; itatetemeka na kuogopa kwa sababu ya kutikiswa kwa mkono wa BWANA wa majeshi, autikisao juu yake.[#Zab 48:6; Isa 30:17; Yer 30:5,7; Nah 3:13]

17Na nchi ya Yuda itakuwa kitisho kwa Misri; kila mtu atakayeambiwa habari zake ataingiwa na woga, kwa sababu ya kusudi la BWANA wa majeshi, analolikusudia juu yake.

Misri, Ashuru na Israeli wabarikiwa

18Katika siku hiyo itakuwako miji mitano katika nchi ya Misri itumiayo lugha ya Kanaani, na kumwapia BWANA wa majeshi; mji mmoja utaitwa Mji wa jua.

19Katika siku hiyo itakuwako madhabahu katika nchi ya Misri kwa BWANA, na nguzo mpakani mwake kwa BWANA.[#Mwa 12:7; Kut 24:4; Yos 22:10; Ebr 13:10]

20Nayo itakuwa ishara na ushuhuda kwa BWANA wa majeshi katika nchi ya Misri; kwa maana watamlilia BWANA kwa sababu ya watu wawaoneao, naye atawapelekea mwokozi wa kuwatetea, naye atawaokoa.[#Yos 4:20; Isa 55:13]

21Na BWANA atajulikana na Misri, na Wamisri watamjua BWANA katika siku hiyo; naam watamtumikia kwa dhabihu na matoleo, nao watamwekea BWANA nadhiri, na kuzitekeleza.[#Mal 1:11]

22Naye BWANA atapiga Misri, akipiga na kuponya; nao wakirudi kwa BWANA, atakubali maombi yao na kuwaponya.

23Katika siku hiyo itakuwako njia kuu itokayo Misri na kufika hadi Ashuru; Mwashuri atafika Misri, na Mmisri atafika Ashuru, na Wamisri wataabudu pamoja na Waashuri.[#Isa 11:15]

24Katika siku hiyo Israeli atakuwa wa tatu pamoja na Misri na Ashuru, watakuwa baraka katika dunia;

25kwa kuwa BWANA wa majeshi amewabariki, akisema, Wabarikiwe watu wangu Misri; na wewe Ashuru, kazi ya mikono yangu; na wewe Israeli, urithi wangu.[#Zab 100:3; Hos 2:23; Rum 3:29; Efe 2:10; Flp 1:6]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya