Isaya 25

Isaya 25

Sifa kwa kukombolewa katika udhalimu

1Ee BWANA, wewe u Mungu wangu;[#Kut 15:2; Hes 23:19]

Nitakutukuza na kulihimidi jina lako;

Kwa kuwa umetenda mambo ya ajabu,

Mashauri ya kale, kwa uaminifu na kweli.

2Kwa sababu umefanya mji kuwa ni rundo;[#Yer 51:37]

Mji wenye boma kuwa ni magofu;

Jumba la wageni kuwa si mji;

Hautajengwa tena milele.

3Kwa hiyo watu walio hodari watakutukuza,[#Ufu 11:13]

Miji ya mataifa yatishayo itakuogopa.

4Maana umekuwa ngome ya maskini,[#Zab 46:1-11; Nah 1:7]

Ngome ya mhitaji katika dhiki yake,

Mahali pa kukimbilia wakati wa tufani,

Na kivuli wakati wa joto;

Wakati kishindo cha watu wakatili kilipokuwa,

Kama dhoruba ipigayo ukuta.

5Kama vile joto katika mahali pakavu

Utaushusha mshindo wa wageni;

Kama ilivyo joto kwa kivuli cha wingu,

Wimbo wa hao watishao utashushwa.

6Na katika mlima huu BWANA wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana.[#Mit 9:2; Mt 22:4; Dan 7:14; Mt 8:11]

7Naye katika mlima huu atauharibu utando uliowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote.[#2 Kor 3:15; Efe 1:17]

8Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana BWANA amenena hayo.[#Isa 26:19; Hos 13:14; 2 Kor 5:4; Ebr 2:14; Mwa 49:18; Tit 2:13; 1 Kor 15:54; Ufu 7:17; 21:4]

9Katika siku hiyo watasema,

Tazama, huyu ndiye Mungu wetu,

Ndiye tuliyemngoja atusaidie;

Huyu ndiye BWANA tuliyemngoja,

Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.

10Kwa maana mkono wa BWANA utatulia katika mlima huu, na Moabu atakanyagwa chini huko aliko, kama vile majani makavu yakanyagwavyo katika maji machafu.[#Isa 15:1—16:14; Yer 48:1-47; Eze 25:8-11; Amo 2:1-3; Sef 2:8-11]

11Naye atanyosha mikono yake katikati yake, kama vile aogeleaye anyoshavyo mikono yake ili aogelee, naye atashusha kiburi chake, pamoja na hila za mikono yake.[#Ayu 40:11,12; Isa 2:10-12,15-17]

12Na boma la ngome ya kuta zako ameliinamisha, na kulilaza chini, na kulitupa chini hadi mavumbini.[#Isa 26:5]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya