The chat will start when you send the first message.
1Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda;
Sisi tunao mji ulio na nguvu;
Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma.
2Fungueni malango yake,[#Zab 118:19; Isa 60:11; Ufu 21:13,24-27]
Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie.
3Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea
Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.
4Mtumainini BWANA siku zote
Maana BWANA YEHOVA ni mwamba wa milele.
5Kwa kuwa amewashusha wakaao juu,
Mji ule ulioinuka, aushusha,
Aushusha hadi chini, auleta hadi mavumbini.
6Mguu utaukanyaga chini,
Naam, miguu yao walio maskini,
Na hatua zao walio wahitaji.
7Njia yake mwenye haki ni unyofu;[#Kum 32:4]
Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki.
8Naam, katika njia ya hukumu zako[#Zab 18:22; Isa 64:5; Mal 4:4; Lk 1:6]
Sisi tumekungoja, Ee BWANA;
Shauku ya nafsi zetu inaelekea
Jina lako na ukumbusho wako.
9Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku;[#Zab 63:6; 83:16; Wim 3:1; Lk 6:12]
Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema;
Maana hukumu zako zikiwapo duniani,
Watu wakaao duniani hujifunza haki.
10Mtu mbaya ajapofadhiliwa,[#Mhu 8:12; Rum 2:4; Zab 143:10]
Hata hivyo hatajifunza haki;
Katika nchi ya unyofu atatenda udhalimu,
Wala hatauona utukufu wa BWANA.
11BWANA, mkono wako umeinuliwa, lakini hawaoni; lakini watauona wivu wako kwa ajili ya watu wako, nao watatahayari; naam, moto utawala adui zako.[#Ayu 34:27; Ebr 10:27]
12BWANA, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote.
13Ee BWANA, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametumiliki; lakini kwa msaada wako peke yako tutalitaja jina lako.[#Zab 66:12]
14Wao wamekufa, hawataishi; wamekwisha kufariki, hawatafufuka; kwa sababu hiyo umewajia, na kuwaangamiza, na kuupoteza ukumbusho wao.
15Umeliongeza hilo taifa, BWANA, umeliongeza taifa; wewe umetukuzwa, umeipanua mipaka yote ya nchi hii.
16BWANA, katika taabu zao walikwenda kwako; waliomba maombi mengi wakati adhabu yako ilipokuwa juu yao.[#2 Nya 33:12; Hos 5:15]
17Kama vile mwanamke mwenye mimba anayekaribia wakati wake wa kuzaa, alivyo na uchungu na kulia kwa sababu ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa sisi mbele zako, Ee BWANA.
18Tumekuwa na mimba, tumekuwa na uchungu, tumekuwa kana kwamba tumezaa upepo; hatukufanya wokovu wowote duniani, wala hawakuanguka wakaao duniani.[#Zab 17:14]
19Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa.[#Isa 25:8; Hos 13:14; Yn 5:28,29; Dan 12:2]
20Njooni, watu wangu, ingia wewe ndani ya vyumba vyako, ukafunge mlango nyuma yako ujifiche kitambo kidogo, mpaka ghadhabu hii itakapopita.[#Mwa 7:1; Zab 30:5; 2 Kor 4:17]
21Kwa maana, tazama, BWANA anakuja kutoka mahali pake, ili kuwaadhibu wakaao duniani, kwa sababu ya uovu wao; ardhi nayo itafunua damu yake, wala haitawafunika tena watu wake waliouawa.[#Mik 1:3; Yud 1:14]