Isaya 29

Isaya 29

Kuzingirwa kwa Yerusalemu

1Ole wa Arieli, Arieli, mji ambao Daudi alifanya kituo chake ndani yake; ongezeni mwaka baada ya mwaka; sikukuu na zirudi wakati wake,

2ndipo nitamwudhi Arieli; kutakuwapo maombolezo na kilio; naye atakuwa kwangu kama Arieli.

3Nami nitapiga kimo juu yako pande zote, nitakuhusuru kwa ngome, nami nitajenga maboma yakuzunguke.

4Nawe utashushwa, nawe utanena toka chini ya nchi, na maneno yako yatakuwa chini toka mavumbini; na sauti yako itakuwa kama sauti ya mtu mwenye pepo, ikitoka katika nchi, na matamko yako yatanong'ona toka mavumbini.[#Isa 8:19]

5Lakini wingi wa adui zako utakuwa kama mavumbi laini, na wingi wao watishao utakuwa kama makapi yapitayo; naam, itakuwa mara na kwa ghafla.

6Naye atajiliwa na BWANA wa majeshi kwa ngurumo, na tetemeko la nchi, na sauti kuu, na chamchela, na tufani, na mwali wa moto uteketezao.

7Na wingi wa mataifa wapiganao na Arieli, wote wapiganao naye na ngome yake, na wanaomwudhi, watakuwa kama ndoto, na maono ya usiku.

8Tena itakuwa kama mtu mwenye njaa aotapo, kumbe, anakula; lakini aamkapo, nafsi yake haina kitu; na kama mtu mwenye kiu aotapo, kumbe, anakunywa; lakini aamkapo, kumbe, anazimia, na nafsi yake inatamani; hivyo ndivyo utakavyokuwa huo wingi wa mataifa waletao vita juu ya mlima Sayuni.

9Ngojeni mstaajabu; fanyeni anasa zenu na kuwa vipofu; wamelewa wala si kwa mvinyo; wamewayawaya wala si kwa sababu ya kileo.

10Kwa maana BWANA amewamwagieni roho ya usingizi, amefumba macho yenu, yaani, manabii; amefunika vichwa vyenu, yaani, waonaji.[#Mik 3:6; 2 The 2:10; Zab 69:23; Isa 6:10; Rum 11:8]

11Na maono yote yamekuwa kwenu kama maneno ya kitabu kilichotiwa mhuri, ambacho watu humpa mtu aliye na maarifa, wakisema, Tafadhali ukisome hiki; akasema, Siwezi, kwa kuwa kimetiwa mhuri;[#Dan 12:4; Mt 11:25; Ufu 5:1]

12kisha kitabu hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi.

13Bwana akanena, Kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walichonacho kwangu ni maagizo ya wanadamu waliyofundishwa;[#Zab 17:1; Isa 48:1,2; Yer 12:2; Eze 33:31; Mt 6:5; Kol 2:22; Mt 15:8-9; Mk 7:6-7]

14kwa sababu hiyo mimi nitafanya tena kazi ya ajabu kati ya watu hawa, kazi ya ajabu na mwujiza; na akili za watu wao wenye akili zitapotea, na ufahamu wa wenye busara wao utafichwa.[#Yer 49:7; 1 Kor 1:19]

15Ole wao wanaojitahidi kumficha BWANA mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? Nani atujuaye?[#Ayu 22:13,14; Zab 10:11,13]

16Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?[#Zab 94:9; Isa 45:9; Rum 9:20]

Matumaini ya siku zijazo

17Je! Si muda mdogo uliobaki, na Lebanoni itageuzwa kuwa shamba lizaalo sana, na lile shamba lizaalo sana litahesabiwa kuwa msitu?

18Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho kitabu, na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza.

19Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika BWANA, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli.[#Yn 15:11; Yak 2:5]

20Kwa maana mwenye kutisha ameangamizwa, naye mwenye dharau amekoma, nao wote watazamiao uovu wamekatiliwa mbali;[#Mik 2:1]

21hao wamfanyao mtu kuwa amekosa katika neno, na kumtegea mtego yeye aonyaye langoni, na kumgeuza mwenye haki kwa kitu kisichofaa.[#Amo 5:10; Mit 28:21]

22Basi, BWANA aliyemkomboa Abrahamu asema hivi, kuhusu nyumba ya Yakobo; Yakobo hatatahayarika sasa, wala uso wake hautabadilika rangi yake.[#Yos 24:3]

23Bali atakapowaona watoto wake, walio kazi ya mikono yangu, katikati yake, wao watalitakasa jina langu; naam, watamtakasa Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli.[#Isa 19:25; Efe 2:10; 1 Pet 4:11; Hos 3:5]

24Hao nao wakosao rohoni mwao watapata kufahamu, na hao wanung'unikao watakubali mafunzo.[#Isa 28:7]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya