Isaya 30

Isaya 30

Ubatili wa kuwategemea Wamisri

1Ole wa watoto waasi; asema BWANA; watakao mashauri lakini hawayataki kwangu mimi; wajifunikao kifuniko lakini si cha roho yangu; wapate kuongeza dhambi juu ya dhambi;[#Kum 29:19; Rum 2:5; 2 Tim 3:13]

2waendao kuteremkia Misri wala hawakuuliza kinywani mwangu; ili wajitie nguvu kwa nguvu za Farao, na kutumainia kivuli cha Misri.[#Hes 27:21; 1 Fal 22:7; Yer 21:2]

3Basi, nguvu za Farao zitakuwa aibu yenu, na kutumainia kivuli cha Misri kutakuwa aibu yenu.[#Yer 37:5,7]

4Kwa maana wakuu wake wako Soani, na wajumbe wake wamefika Hanesi.

5Wote watawaonea haya watu wasioweza kuwafaidia, wasio na msaada wala faida, bali ni aibu na sababu ya kushutumiwa.[#Yer 2:36]

6Ufunuo juu ya wanyama wa Negebu.[#Hos 8:9]

Katikati ya nchi ya taabu na dhiki,

Ambayo hutoka huko simba jike na simba angurumaye,

Nyoka na joka la moto arukaye,

Huchukua mali zao mabegani mwa punda wachanga,

Na hazina zao juu ya nundu za ngamia

Waende kwa watu ambao hawatawafaa kitu.

7Kwa maana msaada wa Misri haufai kitu na ni bure;[#Yer 37:7]

Kwa hiyo nimemwita, “Rahabu aketiye kimya”.

Watu waasi

8Haya, nenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele.[#30:8 Au, majira yatakayokuja, hata milele na milele.]

9Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA;[#Kum 32:20]

10wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;[#Yer 11:21; 1 Fal 22:13]

11tokeni katika njia, geukeni mtoke katika mapito; mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu.[#Mdo 13:8]

12Basi kwa ajili ya hayo Mtakatifu wa Israeli asema hivi, Kwa sababu mwalidharau neno hili, na kutumainia jeuri na ukaidi, na kuyategemea hayo;

13basi, uovu huu utakuwa kwenu kama mahali palipobomoka, kuanguka patokezapo katika ukuta mrefu, ambapo kuvunjika kwake huja ghafla kwa mara moja.

14Naye atapavunja kama chombo cha mfinyanzi kivunjwavyo, kinavyovunjwavunjwa kikatili, hata hakipatikani katika vipande vyake kigae kitoshacho kutwaa moto jikoni, au kuteka maji kisimani.[#Zab 2:9; 2 Pet 2:4,5]

15Kwa maana Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali.[#Isa 7:4; Zab 81:11; Mit 1:24; Yer 44:16; Mt 23:37]

16Bali ninyi mlisema, La! Maana tutakimbia juu ya farasi; basi, ni kweli, mtakimbia; tena, Sisi tutakimbia juu ya wanyama waendao upesi; basi, wale watakaowafuatia watakuwa wepesi.

17Elfu moja watakimbia kwa kukemewa na mtu mmoja; kwa kukemewa na watano mtakimbia; hata mtakapoachwa kama mlingoti juu ya kilele cha mlima, na kama bendera juu ya kilima.[#Law 26:8; Kum 28:25; Yos 23:10]

Ahadi ya Mungu kwa Sayuni

18Kwa ajili ya hayo BWANA atangoja, ili awaonee huruma, na kwa ajili ya hayo atatukuzwa, ili awarehemu; kwa maana BWANA ni Mungu wa hukumu; heri wote wamngojao.[#2 Pet 3:9; Zab 2:12; Mit 16:20; Yer 17:7]

19Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu.

20Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako;

21na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto.[#Kum 5:32; Yos 1:7; 2 Fal 22:2; Mit 4:27]

22Nanyi mtakitia najisi kifuniko cha sanamu zenu za fedha zilizochongwa, na mabamba ya sanamu zenu za dhahabu zilizoyeyushwa; utazitupilia mbali kama kitu kilicho najisi; utasema, Haya, toka hapa.[#2 Nya 31:1; Isa 2:20]

23Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng'ombe wako watakula katika malisho mapana.[#Mt 6:33; 1 Tim 4:8]

24Ng'ombe pia na wanapunda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo.

25Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara.

26Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile BWANA atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha lao.[#Isa 60:19; Zek 2:5; Ufu 21:23]

Hukumu kwa Ashuru

27Tazama, jina la BWANA linakuja kutoka mbali sana, linawaka kwa hasira yake, kwa moshi mwingi sana unaopaa juu; midomo yake imejaa ghadhabu, na ulimi wake ni moto uangamizao;

28na pumzi yake ni kijito kifurikacho, kifikacho hata shingoni, kupepeta mataifa kwa ungo wa ubatili; na lijamu ikoseshayo itakuwa katika taya za watu.[#2 The 2:8]

29Mtakuwa na wimbo kama vile wakati wa usiku, ishikwapo sikukuu takatifu, mtakuwa na furaha ya moyo kama vile mtu aendapo na filimbi katika mlima wa BWANA, aliye Mwamba wa Israeli.

30Naye BWANA atawasikizisha watu sauti yake ya utukufu, naye atawaonesha jinsi mkono wake ushukavyo, na ghadhabu ya hasira yake, na mwako wa moto uangamizao, pamoja na dhoruba, na tufani, na mvua ya mawe ya barafu.

31Maana kwa sauti ya BWANA, Mwashuri atavunjikavunjika, yeye apigaye kwa bakora.

32Na kila pigo la fimbo iliyoamriwa, ambayo BWANA ataliweka juu yake, litakuwa pamoja na matari na vinanda, na kwa mapigano yenye kutikisa atapigana nao.

33Maana Tofethi imewekwa tayari tokea zamani, naam, imewekwa tayari kwa mfalme huyo; ameifanya kubwa, inakwenda chini sana; tanuri yake ni moto na kuni nyingi; pumzi ya BWANA, kama mto wa kiberiti, huiwasha.[#Yer 7:31]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya