Isaya 33

Isaya 33

Unabii wa kukombolewa kutoka kwa watesi

1Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe.[#Hab 2:8; Ufu 13:10]

2Ee BWANA, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu kila asububi, na wokovu wetu pia wakati wa taabu.[#33:2 Au, mkono wao.]

3Makabila ya watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako.

4Na mateka yako yatakukusanywa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige.

5BWANA ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki.[#Zab 97:9]

6Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha BWANA ni hazina yake ya akiba.[#Mit 1:7; Mt 6:33]

7Angalia, mashujaa wao wanalia nje, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.[#2 Fal 18:18]

8Njia kuu zimeachwa, msafiri ameikimbia barabara; ameyavunja maagano, ameidharau miji, hamjali mtu.[#Amu 5:6; 2 Fal 18:14]

9Nchi inaomboleza, na kulegea; Lebanoni imetahayarika na kunyauka; Sharoni imekuwa kama jangwa; Bashani na Karmeli zimepukutika majani.

10Basi, sasa nitasimama; asema BWANA; sasa nitajiinua, sasa nitajitukuza.[#Kum 32:36,43; Zab 12:5; Isa 42:13,14; Sef 3:8]

11Ninyi mtachukua mimba ya makapi, mtazaa majani makavu; pumzi yenu ni moto utakaowateketeza wenyewe.

12Nao mataifa watakuwa kama kuchoma chokaa, kama miiba iliyokatika, iteketezwayo motoni.

13Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uwezo wangu.

14Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uangamizao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?

15Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung'utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za umwagaji wa damu; afumbaye macho yake asitazame uovu.

16Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma.

Nchi ya mfalme mkuu

17Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana.

18Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? Yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? Yuko wapi yeye aliyeihesabu minara?[#1 Kor 1:20]

19Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuielewa.[#Yer 5:15]

20Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa makao ya raha; hema isiyotikisika; vigingi vyake havitang'olewa, wala kamba zake hazitakatika.

21Bali huko BWANA atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo.[#Zek 2:5]

22Kwa maana BWANA ndiye mwamuzi wetu; BWANA ndiye mfanya sheria wetu; BWANA ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa.[#Zab 44:4; Mt 21:5; Ufu 19:16]

23Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka.

24Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.[#Isa 12:2; Rum 11:27]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya