The chat will start when you send the first message.
1Karibuni, enyi mataifa, mpate kusikia; sikilizeni, enyi makabila ya watu; dunia na isikie, na chote kiijazacho, ulimwengu na vitu vyote viutokavyo.
2Maana BWANA ana ghadhabu juu ya mataifa yote, na hasira kali juu ya jeshi lao lote; amewaangamiza kabisa, amewatoa waende kuchinjwa.
3Watu wao waliouawa watatupwa nje, na uvundo wa maiti zao utapaa juu, na milima itayeyushwa kwa damu yao.
4Na jeshi lote la mbinguni litafumuliwa, na mbingu zitakunjwa kama karatasi, na jeshi lao lote litanyauka kama vile jani la mzabibu linyaukavyo na kupukutika, na kama jani la mtini linyaukavyo na kupukutika.[#Zab 102:26; Eze 32:7; Yoe 2:31; 2 Pet 3:10; Mt 24:29; Mk 13:25; Lk 21:26; Ufu 6:13-14]
5Maana upanga wangu umekunywa na kushiba mbinguni; tazama, utashukia Edomu, na juu ya watu wa laana yangu, ili kuwahukumu. Oba 1-14; Mal 1:2-5[#Mal 1:4; Isa 63:1-6; Yer 49:7-22; Eze 25:12-14; 35:1-15; Amo 1:11-12]
6Upanga wa BWANA umeshiba damu, umejazwa mafuta, kwa damu ya wana-kondoo na mbuzi, kwa mafuta ya figo za kondoo dume; maana BWANA ana dhabihu huko Bozra, machinjo makubwa katika nchi ya Edomu.[#Isa 63:1; Sef 1:7]
7Na nyati watateremka pamoja nao, na ndama pamoja na mafahali, na nchi yao italewa kwa damu, na mavumbi yake yatanoneshwa kwa shahamu.
8Maana ni siku ya kisasi cha BWANA, mwaka wa malipo, ili kushindania Sayuni.
9Na vijito vyake vitageuzwa kuwa lami, na mavumbi yake yatageuzwa kuwa kiberiti, na ardhi yake itakuwa lami iwakayo.
10Haitazimwa mchana wala usiku, moshi wake utapaa milele; tangu kizazi hadi kizazi itakuwa ukiwa; hapana mtu atakayepita kati yake milele na milele.[#Ufu 14:11; 19:3]
11Kozi na nungunungu wataimiliki, bundi na kunguru watakaa huko, naye atanyosha juu yake kamba ya ukiwa na timazi ya utupu.
12Watawaitia wakuu wake ufalme, lakini hawatakuwapo; wakuu wake wote wamekuwa si kitu.
13Miiba itamea majumbani mwake, upupu na mbigili ndani ya maboma yake; nayo itakuwa kao la mbweha, na ua la mbuni.[#Isa 32:13; Hos 9:6]
14Na hayawani wa nyikani watakutana na mbwamwitu, na beberu anamwita mwenziwe; naam, babewatoto anakaa huko na kupata pahali pa kustarehe.
15Huko bundi atajenga kiota chake na kutaga mayai na kuyaatamia, na kuangua, na kukusanya vifaranga wake katika kivuli chake; naam, huko watakusanyika tai, kila mmoja na mwenzake.
16Tafuteni katika kitabu cha BWANA mkasome; hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapana mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa changu kimeamuru, na roho yake imewakusanya.[#Zab 56:8; Dan 7:10; Mal 3:16]
17Naye amewapigia kura, na mkono wake umewagawanyia kwa kamba; wataimiliki hata milele, watakaa ndani yake kizazi hata kizazi.[#Zab 78:55; Mit 16:33]