The chat will start when you send the first message.
1Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi.
2Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa BWANA, ukuu wa Mungu wetu.
3Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yaimarisheni magoti yaliyolegea.[#Ayu 4:3,4; Ebr 12:12]
4Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.
5Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa.[#Isa 29:18; Yn 9:6; Mt 9:27; 11:5; Mk 7:32; Lk 7:22]
6Ndipo mtu aliye kilema atarukaruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani.[#Lk 7:22; Yn 5:8; Mdo 3:2; Mt 9:32; Yn 7:38]
7Na mchanga ung'aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi.
8Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.[#Yoe 3:17; Ufu 21:27]
9Hapo hapatakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapanda juu yake; hawataonekana hapo; bali waliokombolewa watakwenda katika njia hiyo.[#Law 26:6; Isa 11:9]
10Na hao waliokombolewa na BWANA watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitatoweka.[#Isa 51:11; 25:8; Efe 1:7; Ufu 7:17; Yn 16:22]