The chat will start when you send the first message.
1Lakini sasa, BWANA aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.[#Isa 44:6; 42:6; 1 Kor 1:9; 2 Tim 1:9]
2Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.[#Zab 66:12; Kum 31:6-8; Dan 3:25]
3Maana mimi ni BWANA, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako.[#Mit 21:18]
4Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na makabila ya watu kwa ajili ya maisha yako.[#Kut 19:5,6]
5Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi;[#Isa 41:10,14; 44:2]
6nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia.
7Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.[#Isa 63:19; 29:23; Zab 100:3; Yn 3:3; 2 Kor 5:17; Efe 2:10]
8Walete watu wasioona, japo wana macho, wasiosikia japo wana masikio.[#Isa 6:9; 42:19]
9Na wakusanyike mataifa yote, kabila zote wakutanike; ni nani miongoni mwao awezaye kuhubiri neno hili, na kutuonesha mambo ya zamani? Na walete mashahidi wao, wapate kuhesabiwa kuwa na haki; au na wasikie, wakaseme, Ni kweli.
10Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine.[#Yn 1:7; Mdo 1:8; Ebr 12:1; Ufu 1:5; Isa 44:8; 41:8]
11Mimi, naam, mimi, ni BWANA, zaidi yangu mimi hapana mwokozi.
12Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, nami ni Mungu.[#Kum 32:16]
13Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hakuna awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?[#Zab 90:2; Mit 8:23; Mik 5:2; Mt 19:26]
14BWANA, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia.
15Mimi ni BWANA, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu.[#Hos 13:10]
16BWANA asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu;[#Zab 77:19]
17atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa kama utambi.[#Kut 14:4]
18Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.
19Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.[#2 Kor 5:17; Ufu 21:5]
20Wanyama pori wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu;[#Isa 48:21; Lk 1:74; Efe 1:5]
21watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.
22Lakini hukuniita, Ee Yakobo, bali umechoka nami, Ee Israeli.[#Mal 1:13]
23Hukuniletea wana-kondoo kuwa kafara zako, wala hukuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukutumikisha kwa matoleo, wala sikukuchosha kwa ubani.
24Hukuninunulia manukato kwa fedha, wala hukunishibisha kwa mafuta ya sadaka zako; bali umenitumikisha kwa dhambi zako, umenichosha kwa maovu yako.[#Isa 1:14; Mal 2:17; Yud 1:4]
25Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.[#Isa 44:22; Yer 31:34; Mik 7:18,19; Eze 36:22]
26Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.
27Baba yako wa kwanza alifanya dhambi, na wakalimani wako wameniasi.[#Rum 5:12]
28Kwa hiyo nitawatia unajisi wakuu wa patakatifu, nami nitamfanya Yakobo kuwalaani, na Israeli kuwa tukano.[#Isa 47:6; Omb 2:2; Zab 79:4; Yer 24:9; Dan 9:11; Zek 8:13]